2013-08-01 12:03:42

Vijana wa kizazi kipya noma!


Queen Said ni Mratibu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio nchini Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, vijana wa kizazi kipya kwa sasa wamemezwa mno na malimwengu, wanajitafuta wao wenyewe na hata wakati mwingine, wanashindwa kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya watu wanaowazunguka. RealAudioMP3

Hawa ni wazee, watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wale ambao jamii inawataza kwa jicho la kengeza!

Vijana wanapaswa kutambua umuhimu wa kujihusisha na matatizo na mahangaiko ya jirani zao, vinginevyo, Jamii itakuwa inaunda vijana wa kizazi kisichojali wala kuguswa na matatizo ya wengine, jambo ambalo ni hatari kabisa kwa sasa na kwa siku za usoni. Vijana wengi wamegubikwa na uchu wa mali, fedha, sifa na tamaa za ujana kiasi kwamba, sasa imekuwa ni nongwa au kwa maneno ya vijana wenyewe imekuwa ni "noma".

Queen Said anasema, Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini lakini zaidi vijana kujenga na kuimarisha utamaduni wa kujali na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati.

Vijana wajifunze kujitosa kimasomaso bila hata ya kujibakiza chembe kwa ajili ya Mungu na jirani zao; vijana waonje na kuguswa na umaskini wa ndugu zao katika Kristo, kama anavyoendelea kukazia Baba Mtakatifu Francisko. Vijana wanachangamotishwa kumwilisha yale waliyojifunza kutoka katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, kwa kukumbatia mafundisho ya Kristo na changamoto zake, ili kwenda ulimwenguni kote kuwafanya mataifa kuwa ni wanafunzi wa Yesu.

Queen Said anasema ni mwaliko na changamoto kwa vijana kurudi ndani ya Kanisa ili kumjifunza tena Yesu Kristo, kwa kumwilisha mafundisho na vipaumbele vyake katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hadi miisho ya dunia. Nchini Tanzania, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inatekeleza utume wake miongoni mwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kule Mwenge, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Kituo cha Wazee Funga funga kilichoko Jimbo Katoliki Morogoro; inawahudumia pia watoto waliofungwa kwenye gereza la watoto watukutu, Manispaa ya Mbeya.

Queen Said anabainisha kwamba, vijana ni chachu ya maendeleo, mabadiliko na furaha katika Jamii, wakitaka wanaweza kumwilisha tunu hizi katika uhalisia wa maisha, changamoto kwa kila kijana kujitoa kwa ajili ya wengine, ili kujenga na kudumisha dunia ambayo ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.









All the contents on this site are copyrighted ©.