2013-08-01 11:02:46

Vatican inaunga mkono huduma msingi kwa wote dhana inayotekelezwa kwa vitendo!


Kanisa ni taasisi ambayo imejitosa kimasomaso kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu: kiroho na kimwili. Majadiliano kuhusu upatikanaji wa huduma makini za afya sanjari na mabadiliko ya idadi ya ongezeko la watu ni jambo muhimu. RealAudioMP3

Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, Jumuiya ya Kimataifa mara nyingi inapozungumza kuhusu masuala ya afya, wasi wasi kuhusu idadi ya watu unajitokeza, hali ambayo inapotosha mwelekeo wa huduma kwa watu kiasi kwamba, huduma hii inaonekana kana kwamba, inapania kudhibiti ongezeko la watu badala ya kuboresha huduma kwa watu wanaohitaji.

Ni mchango wa Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni wakati alipokuwa anashiriki mjadala kuhusu afya na mabadiliko ya idadi ya watu duniani. Vatican inaunga mkono huduma msingi za afya kwa wote; dhana inayotekelezwa na Kanisa kwa njia ya Mashirika yake yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia.

Hadi sasa Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa wa huduma katika sekta ya afya. Inamiliki na kuendesha hospitali 5, 400; Zahanati 17, 500; nyumba za wagonjwa wa Ukoma ni 567 na idadi ya nyumba za wazee na walemavu imefikia nyumba 15, 700.

Hizi ni juhudi za Kanisa kuhakikisha kwamba, linatoa huduma ya afya kwa idadi kubwa ya watu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo kinapomfika kadiri ya mpango wa Mwenyezi Mungu. Vatican inapenda kuchangia kwa kina na mapana katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu mara baada ya Mwaka 2015, uliotengwa maalum na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia.

Ni matumaini ya Askofu mkuu Chullikatt kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kujifunza mafanikio na changamoto kutoka katika Taasisi hizi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Malengo Mapya hayana budi kuvuka mipaka ya kuifanya sekta ya afya kujihusisha na mipango ya uzazi salama ambayo kimsingi inakumbatia utamaduni wa kifo badala ya kutoa huduma ya afya inayopania kulinda na kudumisha zawadi ya maisha.

Kuna zaidi ya watoto 19, 000 kila mwaka wanapoteza maisha kutokana na magonjwa ambayo yangeweza kuzuilika au kutibika. Ni asilimia 25% ya wagonjwa wa Ukimwi wanaopata msaada wa dawa za kurefusha maisha na wengi wao wanatibiwa kwenye Hospitali zinazomilikiwa na kuongozwa na Taasisi za Kidini. Kuna zaidi ya watu millioni 1.4 wanaopoteza maisha yao kila mwaka kutokana na ugonjwa wa Malaria na Kifua Kikuu. Ukosefu wa huduma msingi za afya ni mzigo kwa nchi changa zaidi duniani, ambako kuna zaidi ya watu millioni 100 wanaoteseka kutokana na umaskini wa hali na kipato pamoja na kukabiliana na gharama kubwa ya huduma ya afya.

Askofu mkuu Chullikatt anabainisha kwamba, dunia ina rasilimali fedha na vifaa ambavyo vingeweza kuokoa maisha ya mamillioni ya wagonjwa, lakini, bado hakuna utashi wa kisiasa katika utekelezaji wa changamoto hii kutokana na baadhi ya Makampuni kujikita zaidi katika kutafuta faida kubwa badala ya kuguswa na utu pamoja na mahangaiko ya binadamu wanaoteseka kutokana na magonjwa sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja ya kuondokana na ubinafsi na uchu wa mali na utajiri wa haraka harakan a badala yake kujenga mshikamano unaoongozwa n akanuni ya auni ili kuleta maboresho katika sekta ya afya.

Uelewa wa idadi ya watu usaidie kuboresha huduma mbali mbali na kamwe kisiwe ni kigezo cha kuanza kuibua sera na mikakati ya kutaka kuzuia ongezeko la watu duniani kwa kukumbatia utamaduni wa kifo, kwa kudhani kwamba, binadamu ni kikwazo cha maendeleo endelevu! Jamii ambazo zimekumbatia utamaduni wa kifo kwa sasa zinakabiliana na idadi kubwa ya wazee wanaohitaji huduma za kijamii. Kwa upande mwingine, vitendo vya utoaji mimba vimewanyima watu wengi fursa ya kushiriki katika kuchangia maendeleo na ustawi wa nchi zao.

Askofu mkuu Chullikatt anasema, ongezeko la rasilimali fedha lisaidie kulinda na kudumisha zawadi ya uhai kwa kuokoa na kulinda maisha ya mamillioni ya watu wanaofariki dunia kutokana na magonjwa na hivyo kuondokana na dhana ya vidhibiti mimba. Ni kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu kimataifa, changamoto kubwa ni kulinda kwanza maisha!








All the contents on this site are copyrighted ©.