Upendo na uaminifu hukutana pamoja, haki na amani hubusiana!
Jumuiya ya Mtakatifu Agidio yenye makao yake makuu mjini Roma ni familia kubwa ya
waamini walei kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kujitosa kimasomaso
kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na
kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.
Kuanzia tarehe 2 hadi
tarehe 4 Agosti 2013, wawakilishi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio nchini Tanzania wanakutana
Jimbo kuu la Arusha, kama njia ya kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao na wengine
wengi kujeruhiwa wakati bomu liliporushwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Olasti ya Mtakatifu
Yosefu, Mfanyakazi, Jimbo kuu la Arusha hivi karibuni.
Mkutano huu unaongozwa
na kauli mbiu "Upendo na uaminifu hukutana pamoja, haki na amani hubusiana" Zaburi
ya 85. Wanajumuiya wanapenda kuanza mkutano wao kwa kuwakumbuka waathirika wa mabomu
Jimbo kuu la Arusha, kama mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi
ya haki, amani na upatanisho miongoni mwa Jamii.
Wanachama wa Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio wanashiriki katika utekelezaji wa malengo na mikakati ya Jumuiya hii kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa sala, uenezaji wa Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya
utekelezaji wa maisha yao kama wabatizwa. Ni watu wanaohamasishwa kujenga na kudumisha
mshikamano wa dhati na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana
na hali na nafasi yao katika Jamii husika.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican wanaendelea kukazia umuhimu wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda
wa maisha unaojikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, kama njia ya kuhamasisha
mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho miongoni mwa Jamii.