2013-08-01 09:17:47

UNICEF: Watoto milioni 223 wanaathirika kutokana na nyanyaso na dhuluma


Uonevu na nyanyaso dhidi ya watoto ni visa vinavyoyaepuka macho na masikio ya watu wengi kwani mara nyingi havifikishwi kwenye vyombo vya sheria. Haya yamesemwa na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, (UNICEF). Shirika hili limewaomba watu binafsi, wanasheria, na serikali za nchi mbali mbali kutofumbia macho vitendo vya unyanyasaji wa watoto duniani.

Shirika hili linapinga visa vya kinyama na uonevu dhidi ya watoto vinavyozidi kujitokeza kama kile kisa cha kupigwa risasi mtotoMalala Yousafazai huko Pakistani, na kile kisa cha kuwaua kwa risasi watoto 26 na walimu wao kwenye shule moja ya Newton, Connecticut, nchini Marekani mnamo mwezi Desemba, 2012. Matukio mengine ni ya unyanyasaji wa wasichana nchini India na Afrika ya Kusini kwa mwaka 2013.

Mateso dhidi ya watoto ni jambo linaloikabili kila nchi na tamaduni, anasema Mkurugenzi wa UNICEF, Anthony Lake, na kwamba kila mara mtoto yeyote anapokumbwa na mateso mahali popote duniani, watu hawana budi kuonyesha masikitiko yao na kusaidia kuyaleta hadharani mateso haya mengi yakiwa yanatendeka kisiri.

Huu ni ujumbe wa kwanza kwenye kampeni ya UNICEF ya kutaka kusitisha unyanyasaji dhidi ya watoto. Kampeni hii ya kimataifa inawalenga watu wote duniani ili waweze kutambua na kuondokana na visa vya unyanyasaji dhidi ya watoto, ili kujenga utamaduni wa kuwahehimu, kuwathamini na kuwalinda watoto katika malezi na ukuaji wao.

Uzinduzi wa kampeni hii umefanyika kupitia video ambapo Balozi wa Matashi Mema wa UNICEF, Liam Neeson anasikika akiwaongoza watazamaji kuona visa mbalimbali vya unyanyasaji vinavyowakabili watoto kisirisiri. Mfano wa visa hivyo ni pamoja na kile cha ubakaji wa msichana wa miaka 15 mikononi mwa kundi la vibaka; na mtoto anayepigwa hadi kuumizwa vibaya na mwalimu wake kwa kukosa kujibu swali kwa usahihi baada ya kuulizwa na mwalimu wake darasani.

Balozi huyu wa matashi Mema wa UNICEF, Liam Neeson anasema kwamba, kwa vile visa vingi havitendeki hadharani, haimaanishi kwamba havitokei, na anawashawishi watu wote wa mapenzi mema kushiriki katika kampeni hii, ili kuweza kuviweka hadharani visa vyote vinavyotendeka dhidi ya watoto, hata kama vinatendeka katika uficho mkubwa.

Kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani ya Mwaka 2005, zaidi ya watoto milioni 150 wa kike na watoto wengine milioni 73 wa kiume chini ya miaka 18 wamepitia madhulumu na nyanyaso za kijinsia, na kwamba, watoto wengine milioni 1.2 kila mwaka huangukia kwenye soko la biashara haramu ya binadamu.

Inapaswa kukumbukwa kwamba, visa hivi haviachi majeraha mwilini mwa watoto waathirika, bali pia kwenye akili na utu wao kwa ujumla na kwamba, vinaathiri pia uwezo wao wa kuelewa, kukua na kuchangamana na wenzao katika jamii.

Kuwatetea na kuwalinda watoto duniani ni lengo na kiini cha majukumu ya UNICEF. Tamko la Haki za Watoto la Umoja wa Mataifa linafafanua kwamba, kila mtoto, popote pale alipo, ana haki ya kulindwa dhidi ya uonevu na mateso ya aina yoyote ile.
All the contents on this site are copyrighted ©.