2013-08-01 08:11:05

Kampeni inayotafuta haki ya huduma bora za afya na maji safi na salama kwa wote!


Haki ya kupata maji safi na salama pamoja na huduma za afya kwa watu wote duniani hata maskini na walio pembezoni mwa jamii ni jambo lililojadiliwa kwa kina na wajumbe wa mkutano wa kimataifa uliofanyika hivi karibuni mjini Berlin, Ujerumani.
Mkutano huu ulitayarishwa na Tume ya Kiekumene kuhusu Maji ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni ili kuchangamotisha uwezekano wa kupata majibu na vitendo muafaka kwa ajili ya usawa kwenye ugavi na usambazaji wa maji na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji unapewa kipaumbele cha kwanza kwenye ajenda zote zinazolenga mwaka 2015 na kuendelea.
Ni lazima Kanisa liwe msitari wa mbele kwenye majadiliano ya kuhakikisha ndoto ya kupata maji safi na salama kwa watu wote inatimia katika jamii, ilisema hati iliyootolewa na mkutano huo, ambayo iliongozwa na kauli mbiu: “Mungu, tuongoze kwenye uzima wa uhai na amani kupitia Maji”.
Hati hii ilichangiwa na wakuu wa Makanisa 40 wakiwemo: wanataalimungu, wanataaluma na wakereketwa waliofika Berlin kushiriki kwenye mkutano huo. Mwenyeji wa mkutano huu kilikuwa ni kikundi cha Misaada cha Kanisa la Ujerumani kijulikanacho kama Mkate kwa Dunia.
Hati ya mkutano huo iliziomba serikali mbali mbali pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kuafikiana kwenye jukumu la kuhakikisha maji safi na salama, huduma makini za afya zinapatikana kwa watu wote ifikapo mwaka 2030.
Akifungua mkutano huo, Rais wa kikundi cha Mkate kwa Dunia, Kasisi Cornelia Fulkrug-Weitzel alisema, Kikundi chake kiliungana na makundi mengine ya Kiekumene ili kuanzisha harakati za kutetea haki ya maji na akawahakikishia waliohudhuria kwamba, wataendelea kuchangia kwa kina na mapana mijadala na ushauri wa Tume hiyo ya Kiekumene kuhusu haki ya maji.
Naye Maria Francisca Ize-Charin wa Waterlex alisema kuwa, maji ni rasilimali muhimu kwa ajili ya mafao ya wengi na hayawezi kamwe kufanywa kama haki inayomilikiwa na watu wachache ndani ya jamii kwani haki hii inaweza kutumiwa vibaya na makampuni binafsi ya uzalishaji na ugavi wa maji duniani. Makampuni haya yanaweza kumiliki na kubinafsisha vyanzo vya maji, bila kujali wala kuzingatia haki ya wananchi mahalia, jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki msingi za binadamu.
Wengine waliochangaia mawazo kwenye mkutano huo walikuwa Balozi Luis Gallegos, mwakilishi wa kudumu wa nchi ya Ecuardo kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, na Rabbi Awraham Soetendorp wa Jacob Soetendorp Institute for Human Values. Malengo ya Maendeleo ya Milenia pia yaliongelewa kwa kina na Virginia Roaf, Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya haki ya maji safi na afya.
Majadiliano haya yalionesha mwelekeo thabiti kwa Makanisa ili kuweza kuunda mikakati muafaka ya kukabiliana na changamoto za maji, na ya haki ya kupata maji safi na salama. Alisema Makanisa yana nafasi ya kujikita kwenye mchango wa kutetea maendeleo yanayotokana na haki ya maji na ya afya bora.
Tume hii ya Kiekumene kwa ajili ya maji ilipata pia fursa ya kushiriki kwenye mkutano wa Baraza la Makanisa katika maandalizi ya mkutano mkuu utakaofanyika mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini, kuanzia tarehe 30 Oktoba hadi tarehe 8 Novemba 2013.
All the contents on this site are copyrighted ©.