2013-08-01 10:46:37

Hija ya utakatifu wa Yohane Paulo II


Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili ni kiongozi aliyeonesha utakatifu wa maisha hatua kwa hatua, tangu alipokuwa bado ni kijana mbichi kabisa. Ni mtu aliyependa kufurahia zawadi ya maisha na Kristo akapewa kipaumbele cha kwanza katika maisha yake, kiasi kwamba, akabaki mwaminifu hadi mauti yalipomfika, pale dunia ilipopigwa na bumbuwazi na kushika tama! RealAudioMP3

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alikuwa mwaminifu kwa upendo wa Kristo, jambo ambalo lilijionesha kwa namna ya pekee kabisa katika: Sala pamoja na huduma kwa Mungu na jirani. Ni mtu aliyejenga utamaduni wa majadiliano na Muumba pamoja na Mkombozi wake, yaani Yesu Kristo.

Alipenda kukutana na Yesu katika madhabahu ya undani wa moyo wake, akaona ile chapa ya Mungu katika mazingira na maisha ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Akasimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai. Ni kiongozi aliyekuwa anazama katika tafakari ya kina kama sehemu ya matunda ya utume wake kwa Mungu, Kristo na Kanisa.

Hii ni sehemu ya tafakari ya kina iliyotolewa na Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, anaposimuliwa kwa ufupi utakatifu wa maisha ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, ambaye alibahatika kufanya naye kazi kwa miaka arobaini, tangu alipokuwa kijana na sasa taa ya maisha yake inaanza kufifia!

Tarehe 16 Oktoba 1978, utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili uliokuwa umefichika ndani ya Jimbo kuu la Cracovia, ulianza kujionesha taratibu kwa Kanisa la Kiulimwengu hasa zaidi kwa njia ya hija zake za kichungaji, zilizowagusa watu na kuacha chapa ya kudumu hadi leo hii. Alitafakari Neno la Mungu; akahubiri kwa ari na moyo mkuu; akaadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji; akawafundisha waamini Katekesi ya kina kuhusu kweli za Kiinjili.

Aliwaambia vijana ukweli na akata vijana waumwilishe ukweli huu katika maisha yao ya kila siku, wakijitoa kimaso maso kwa ajili ya Mungu na jirani. Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, alitamani utakatifu wa maisha, akaufanyia kazi, hata katika mateso na mahangaiko yake. Akaonesha ujasiri na imani kubwa hata pale alipokabiliana na vizingiti na changamoto za maisha.

Papa Yohane Paulo wa Pili ni mtu aliyekuwa anazungumza kutoka katika undani wa moyo wake, kwa kushirikisha yale yaliyomgusa na kumsibu katika hija ya maisha yake. Alipokuwa anazungumzia kuhusu mateso na mahangaiko ya wagonjwa, alifahamu kile kilichomkuta katika maisha yake, tarehe 13 Mei 1980, risasi ilipopenya mwilini wake, lakini kwa maombezi ya Bikira Maria akakipatia kifo kisogo, na kuliandaa Kanisa kuingia katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, akiwahamasisha waamini na watu wenye mapenzi mema, kutweka hadi kilindini.

Utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili inajikita katika maisha ya kawaida na huduma kwa Mungu, Kanisa na binadamu. Alimwendea Mungu kwa moyo wa unyenyekevu, akatamani kuwapeleka wengine pia kwa Mwenyezi Mungu, daima akisimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ni kiongozi aliyeshuhudia kuta za utengano kati ya watu wa mataifa zikiporomoka na watu kuanza mchakato wa ujenzi wa upendo, mshikamano na udugu! Watu wengi wakaanza kufungua malango ya maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake! Kwa hakika Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, amekuwa ni Jabali la Imani katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Kanisa linamshukuru kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyeridhia mchakato wa kutangazwa kwake kuwa Mwenyeheri, akabahatika kumtangaza na panapo majaliwa ataweza kushuhudia akitangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Francisko. Hapa atakuwa anatia nanga ya utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Kardinali Stanislaw Dziwisz anasema, hataweza kusahau kamwe katika maisha yake, tarehe 18 Aprili 2005 pale alipochukua Sanda na kuufunika uso wa Papa Yohane Paulo wa Pili. Atakapotangazwa kuwa Mtakatifu, itakuwa ni fursa kwa Kanisa zima kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili!

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.