Makanisa yanapania kuendelea kuwasaidia Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu
Kuna umuhimu wa kuisaidia Nchi Takatifu ili iendelee kutimiza majukumu yake ya kutoa
huduma ya upendo kwa watu wanaoishi pembezoni mwa jamii na wahitaji. Haya yamesemwa
hivi karibuni na Askofu Mkuu Justin Welby, wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pia ni
Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani Duniani, alipokutana na wawakilishi wa kundi la
Marafiki wa Nchi Takatifu.
Hili ni kundi la kiekumene ambalo lililoundwa kunako
mwaka 2009, lina makao yake Makuu nchini Uingereza na lina malengo ya kuwasaidia Wakristo
wanaoishi katika Nchi Takatifu. Wakati wa mkutano huo, Askofu Mkuu Welby alikubali
kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu mstaafu Rowan Williams wa Jimbo kuu
la Canterbury, kama mmoja wa wafadhili wa nchi Takatifu. Wafadhili wengine ni
pamoja na Askofu mkuu Vincent Gerard Nichols Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza
na wengi wa marafiki wa Nchi Takatifu ni waamini wa Kanisa la Kiangalikiani nchini
Uingereza. Wafadhili hawa pia hutumia muda wao kuwaombea Wakristo wanaoishi katika
Nchi Takatifu na kupanga hija za kwenda kwenye maeneo matakatifu nchini humo.