Kristo na Kanisa lake apewe kipaumbele cha kwanza na Wayesuit
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Inyasi wa
Loyola, Mwanzilishi wa Shirika la Wayesuit, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kanisa kuu la Gesù liloloko mjini Roma. Ibada hii imehudhuiriwa na Wayesuit, wafanyakazi
na wadau mbali mbali katika maisha na utume wa Wayesuit mjini Roma.
Baba Mtakatifu
katika mauhibiri yake amewataka Wayesuit na wadau wao kumweka Kristo kuwa ni kiini
cha maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu pia amemkumbuka kwa namna
ya pekee, Padre Paolo Dall'Oglio anayetekeleza utume wake nchini Syria, kwa sasa hajulikani
mahali alipo. Wayesuit wanaalikwa kwa namna ya pekee kujitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya Mungu na jirani zao. Hivi ndivyo walivyofanya akina Mtakatifu Francisko Saverio
na Padre Pedro Arupe, aliyekuwa mkuu wa Shirika la Wayesuit kwa miaka mingi.
Baada
ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu amebaki na Wayesuit kwa takribani masaa
mawili, akapata kifungua kichwa pamoja na kuzungumza nao. Kwa Wayesuit hii imekuwa
ni siku maalum sana inayoacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wao kwa Kristo
na Kanisa lake.
Padre Adolfo Nicolas, Mkuu wa Wayesuit anasema, Baba Mtakatifu
ndiye mkuu wala hana tena kifungo cha kuweka nadhiri ya nne ya utii kwa Baba Mtakatifu.
Ni kiongozi huru kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo na wala hakuna mkanganyo
wa uwajibikaji katika masuala ya uongozi. Kwa njia hii, inakuwa ni rahisi kwa Wayesuit
kujenga na kuimarisha umoja na Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada
ya Ibada ya Misa takatifu amekwenda kutoa heshima yake kwenye Kaburi la Mtakatifu
Inyasi, Mtakatifu Francisko Saverio na kaburi la Padre Pedro Arrupe, aliyekuwa ni
kiongozi makini wa Wayesuit.