2013-07-31 15:22:36

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014


Udugu ni msingi na njia ya amani ndiyo kauli mbiu iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014 inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu.

Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani ni jitihada za Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa sita kutaka kuhakikisha kwamba, Kanisa kila mwaka linawatumia wakuu wa nchi na Serikali duniani ujumbe wa amani, kwa kutambua kwamba, wao wanayo dhamana ya kusimama kidete kulinda na kutetea amani duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa kupambana fika dhidi ya utamaduni wa kutojali na badala yake kujenga utamaduni wa kukutana ili kujenga dunia inayosimikwa katika misingi ya haki na amani. Udugu ni amana ambayo kila mtu amekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake, amana inayoweza kusaidia kupambana na umaskini, baa la njaa, ukosefu wa mikakati na msingi wa maendeleo endelevu, kinzani, uhamiaji, ongezeko la watu, ukosefu wa usawa na haki; uhalifu wa kimataifa na misimamo mikali ya kidini. Baba Mtakatifu anasema, udugu ni msingi na njia ya amani.

Huu ni mchakato wa kuhakikisha kwamba, kila mtu anawajibika kujenga na kudumisha udugu ili kubomoa kuta za utengano zinazowafanya baadhi ya watu kujisikia kuwa ni adui na maskini kuonekana kuwa ni mzigo na kikwazo cha maendeleo kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii wanapaswa kuonja upendo na ukarimu kutoka kwa Jamii inayowazunguka. Hawa ni ndugu wanaopaswa pia kushirikishwa zawadi za kazi ya uumbaji, mafanikio ya maendeleo na tamaduni, ili waweze kushiriki kikamilifu katika utimilifu wa maisha sanjari na kuwa ni wadau wa maendeleo endelevu na shirikishi.

Baba Mtakatifu anasema, udugu ni zawadi na dhamana inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo inawakumbatia wote. Inasaidia kujenga misingi ya kupambana na utandawazi usiojali na baadala yake kuanza mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa udugu unaoacha chapa na alama ya kudumu katika medani mbali mbali za maisha: kiuchumi, kifedha, kiraia, katika tafiti, maendeleo maisha ya hadhara na katika taasisi mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuata nyayo za watangulizi wake wanaohimiza njia ya udugu na mshikamano ili dunia iweze kupata taswira ya kibinadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.