2013-07-31 10:46:15

Baada ya vita, madhulumu na nyanyaso kutulia, mikakati inafanywa ili kufanya ukarabati mkubwa Afrika ya Kati


Shirika la Kipapa la Msaada kwa Makanisa hitaji linasema kwamba, tangu Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ilipoingia kwenye vita, kinzani na migogoro ya kijamii; watu zaidi ya 400 wameuwawa kikatili; wanawake na wasichana wengi wamenyanyaswa na kudhulumiwa utu na heshima yao. Kuna wananchi wengi ambao wamelazimika kuyakimbia na kuyahama makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao.

Katika mazingira kama haya, Majimbo 4 ya Kanisa Katoliki yamejikuta kwamba, yamepoteza walau asilimia 50% ya rasilimali yake, kumbe yanapaswa kusaidiwa kuanza upya. Shirika la Kipapa laMsaada kwa Makanisa hitaji limetenga fungu maalum kwa ajili ya ukarabati wa Makanisa na nyumba za Mapadre kwa majimbo manne ya Kanisa Katoliki nchini Afrika ya Kati.

Makanisa mengi yameporwa na kunajisiwa, hali ambayo kwa sasa inakwamisha maisha na utume wa Kanisa Majimboni humo. Haya yamo kwenye taarifa iliyoandikwa na Askofu Juan Josè Aguirre wa Jimbo Katoliki la Bangassou, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.







All the contents on this site are copyrighted ©.