2013-07-30 12:06:16

Wanawake Barani Afrika wanapaswa kutoka kifua mbele ili kusimamia misingi ya haki, amani, utu na heshima ya Mwafrika!


Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka hamsini tangu Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Barani Afrika lilipoanzishwa ni fursa makini ya kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya wanawake Barani Afrika sanjari na kuwajengea uwezo ilikushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Jamii zao. RealAudioMP3

Wanawake Barani Afrika wamekuwa ni waathirika wakubwa wa Ukimwi, nyanyaso na dhuluma kutoka ndani na nje ya familia zao. Miaka hamsini iwe ni nafasi kwa wanawake wa Bara la Afrika kutoka kifua mbele ili kusimamia misingi ya haki na amani na utu wa Mwafrika.

Ni changamoto ambayo imetolewa na Bi Botshelo Moilwa kutoka Botswana, wakati alipokuwa anashiriki katika mkutano wa kumi wa Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Barani Afrika, uliohitimishwa hivi karibuni mjini Kampala, Uganda. Kulinda na kutetea utu na heshima ya mwanamke ni jambo la msingi ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na wadau katika medani mbali mbali za maisha.

Bi Botshelo Moilwa tangu mwaka 2010 amekuwa akijihusisha na huduma kwa watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi. Amekuwa pia mstari wa mbele kuwasaidia wanawake walionyanyaswa na kudhulumia kijinsia nchini Botswana. Anasema, hii ni kati ya changamoto kubwa inayolikabili Bara la Afrika, hii ni kutokana na ukweli kwamba, Jamii nyingi za Kiafrika zimekumbatia mfumo dume, ambao mwanamke si mali kitu mbele ya mwanaume! Wanawake wanatengwa na kubaguliwa, hata kutoka ndani mwa Familia zao wenyewe, kana kwamba, wao si watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Bi Moilwa anakumbusha kwamba, kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wanawake na wanaume wanapaswa kushirikiana ili kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Jamii za Kiafrika zijifunze kuheshimiana na kuthaminiana, kwa kuimarisha mahusiano mema ndani ya Jamii, kwani ile sura na mfano wa Mungu ndani ya mwanadamu ni tunu msingi inayounda uhusiano wa pekee miongoni mwa Jamii.

Kutokana na mwelekeo kama huu, ndiyo Maana Bi Botshelo Moilwa ameweza kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya wanawake nchini Botswana; kwa kuwajengea uwezo kiuchumi pamoja na kuwapatia mbinu za kujikinga na wanaume walaghai wanaoweza kuwaambukiza magonjwa.

Jamii itambue na kuheshimu thamani ya utu wa mtu, kwani hiki ni kielelezo cha utakatifu wa maisha na haki na amani. Kanisa liwe ni mahali ambapo wanawake wanaweza kupata faraja, kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Hapa ni pale mahali ambapo mwanamke anajisikia na kupata utambulisho wake. Kanisa lisaidie mchakato wa kuwapatia wanawake heshima yao kwa kukazia maadili na tunu bora za maisha.

Wanawake wanapaswa nao kuamka na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima yao. Wanawake waliobahatika kukanyaga umande na kuwa na uwezo wa kiuchumi, wawasaidie wanawake wenzao katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, ujinga na maradhi. Wawe mstari wa mbele kupigania haki jamii, ili Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, mahali ambapo: utu, haki na amani vinalindwa na kuthaminiwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.