2013-07-30 09:25:31

Papa achonga na waandishi wa habari kwa muda wa dakika 80 na kujibu hata maswali ya udaku!


Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka kwenye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro, amepata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kuwashukuru kwa kazi kubwa walioifanya katika kuwahabarisha walimwengu kile kilichokuwa kinatendeka huko Brazil.

Anasema, kwake, hija hii ya kichungaji imekuwa na mafao makubwa kiroho na kimwili, kwani imekuwa ni sherehe ya imani miongoni mwa vijana na wananchi wa Brazil, wenye moyo na ukarimu mkubwa. Amezungumzia kuhusu usalama na kwamba, hata katika pilika pilika hizi, alipata nafasi ya kuweza kusalimiana na kuzungumza na wananchi wa Brazil waliokuwa wanafurika katika barabara, ingawa vikosi vya ulinzi na usalama vilikuwa na wasi wasi mkubwa, lakini yote yamekwenda salama salimini kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, anapenda kuwa karibu na watu na hili ni jambo la muhimu sana katika maisha na utume wake. Anasema ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na maadhimisho ya Liturujia, Katekesi, Sanaa na za Maonesho. Ibada kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida ni kati ya mambo ambayo yamebakiza chapa ya kudumu katika maisha yake ya kiroho. Anawashukuru waandishi wa habari kwa kazi kubwa waliyoifanya, ingawa yeye binafsi hakupata nafasi ya kusoma magazeti. Umati wa vijana millioni tatu ni jambo la kushangaza na la kumshukuru Mungu. Hawa walikuwa ni wawakilishi wa vijana kutoka katika nchi 178 duniani.

Baba Mtakatifu akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari anasema, kwa sasa anaendelea kutekeleza utashi wa Makardinali waliouonesha wakati wa mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali walipendekeza kuwa na kundi la Makardinali wanane watakaosaidia kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa dhamana na utume wake kwa Kanisa la ulimwengu katika mwelekeo wa maazimio ya Sinodi.

Kuna mapendekezo ya kufanya mabadiliko katika Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu ili iweze kuwa ni chombo cha kudumu pamoja na kufanya mikutano ya Makardinali mara kwa mara kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa. Mabadiliko ya Benki ya Vatican ni kati ya mambo aliyoyapatia kipaumbele cha kwanza kutokana na unyeti wake na baada ya kikao cha Makardinali, ilionekana kwamba, kulikuwa na haja ya kuunda Tume ambayo ingeweza kuangalia kwa kina na mapana kuhusu masuala ya uchumi wa Vatican. Jambo la msingi anasema Baba Mtakatifu katika masuala ya fedha na uchumi ni lazima yaongozwe na sera ya ukweli na uwazi.

Waandishi wa habari wameulizia pia siri anayoficha kwenye mkoba ambao umekuwa ni gumzo tangu alipoanza hija yake ya kichungaji nchini Brazil! Baba Mtakatifu anasema, haya ni mazoea yake binafsi, daima amejibebea mkoba wake wakati wa safari zake, hili ni jambo la kawaida, changamoto ya kuendelea kuwa ni watu wa kawaida katika unyenyekevu.

Ndani ya Mkoba huu anasema Baba Mtakatifu anachukua Kitabu cha Sala za Kanisa, baadhi ya vitabu anavyopenda kujisomea wakati wa mapumziko na kwamba, anaendelea bado kuwahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya maisha na utume wake. Anaendelea kuishi kwenye Hostel ya Santa Martha iliyoko mjini Vatican kwa sababu anaona umuhimu wa kuishi katika Jumuiya; ili kukutana na kuzungumza na watu.

Kila kiongozi wa Kanisa anapaswa kuishi kadiri inavyotakiwa na Kristo mwenyewe, bila kuonesha makuu kwani kuna watu wanaoteseka kutafuta mahitaji yao ya kila siku, lakini bado wanajitoa sadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hawa ni watu wanaoishi utakatifu katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Hata Vatican kama ilivyo ndani ya Kanisa kuna watakatifu na wadhambi wanaopania kujitakatifuza!

Baba Mtakatifu anasema kuhusu suala la utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja ni mambo ambayo Kanisa limekwishayazungumzia na kuyatolea msimamo wa kimaadili na kiutu, kumbe haikuwa ni lazima kuyazungumzia tena, kama ambavyo hakugusia masuala ya rushwa, wizi na ufisadi kwani yamekwishazungumziwa kwa kina na mapana na msimamo wa Kanisa unaeleweka bayana.

Maamuzi mengine ya maisha yanapania kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kidini kwa ajili ya mafao na ustawi wa watu wa Mungu duniani. Askofu anadhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu anapaswa kuandamana na waamini katika hija ya maisha yao na kamwe hapaswi kuwa ni Mfalme wa kuabudiwa!

Kati ya matukio ambayo yako mbele yake kwa sasa ni hapo tarehe 22 Septemba 2013 atakapotembelea Kisiwa cha Cagliari. Hii itakuwa ni safari ya siku moja. Kuna mwaliko kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza kuhusu Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Patriaki Athenagora alipokutana na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo wa sita, maadhimisho ambayo yamepangwa kufanyika mjini Yerusalemu, bado anafikiria uwezekano wa safari hii. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, hakupata nafasi ya kwenda Barani Asia, hii ni changamoto kwa Papa Francisko kwa sasa. Ana mawazo ya kutembelea Sri Lanka na Ufilippini.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanachama wa vyama vya kitume wanaotekeleza majukumu yao kama sehemu ya mchakato wa kujitajirisha katika maisha ya kiroho, kama wanavyofanya wanachama wa Uamsho wa Roho Mtakatifu. Vyama hivi ni matunda ya Roho Mtakatifu na neema kwa maisha na utume wa Kanisa. Wanachama wanapaswa kusaidiwa kutekeleza wajibu wao kadiri ya mafundisho ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anapongeza mchango unaoendelea kutolewa na Wanawake Wakatoliki ndani ya Kanisa, kwani wamekuwa ni msaada mkubwa katika ukuaji wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ni kundi ambalo lina mchango mkubwa katika kulinda na kudumisha utamaduni, maadili sanjari na kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya. Kanisa limekwishatoa uamuzi wa kutowapatia wanawake daraja takatifu la Upadre. Dhamana na utume wa wanawake unapaswa kufafanuliwa vyema na taalimungu makini na wala si jambo la hisia wala usawa katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa Francisko amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa maamuzi, ujasiri na busara yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Ni mtu wa sala na mfano wa kuigwa na wengi. Ni kiongozi anayepaswa kupendwa, kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusikilizwa kwa makini, kwani ndani mwake anatunza utajiri mkubwa wa maisha na utume wa Kanisa la Kristo. Ni mtu ambaye anamsaidia Papa Francisko katika huduma kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ndani ya Kanisa kuna kashfa, madonda na machungu ya maisha ya kiroho yanayopaswa kuponywa kwa njia ya: toba, msamaha na huruma ya Mama Kanisa. Hivi ndivyo Kanisa linavyochangamotishwa kuwaangalia wanandoa waliotengana na baadaye wakaoana na watu wengine. Kuna haja ya kuwa na mwelekeo makini wa mikakati na shughuli za kichungaji kwa wanandoa watarajiwa bila kusahau majiundo endelevu kwa wanaoishi katika ndoa, ili waweze kutekeleza dhamana na utume waliokabidhiwa na Mama Kanisa pamoja na Jamii katika ujumla wake.

Ndoa na Familia ni mada zinazofanyiwa kazi kwa sasa, ili wanandoa watarajiwa waweze kuwa na ukomavu wa kutosha katika maisha yao kwa kuelewa sheria za nchi na kanuni za Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema yeye anajisikia kuwa ni Myesuiti kutoka katika undani wa maisha na majiundo yake na kwamba, anatarajia kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai. Anasema, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amefurahia kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, amesikitishwa na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi kwenye Kisiwa cha Lampedusa, Kusini mwa Italia. Ameguswa kwa namna ya pekee alipokutana na watoto wanaosoma kwenye shule za Wayesuit na alipokutana na umati wa Waseminari na Wanovisi katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Anasema, anaendelea kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi pamoja na wafanyakazi wa Vatican, jambo ambalo anamshukuru Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alimwelezea kwa ufupi yale yaliyojiri kwenye nyaraka za "Vaticanleak". kwa hakika ni mtu mwenye uwezo na uelewa mkubwa!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, moyoni mwake anasubiri kwa furaha kuwatangaza Mwenyeheri Yohane wa ishirini na tatu na Yohane Paulo wa pili kuwa watakatifu, viongozi wa Kanisa walioacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni watu waliojikita katika maisha ya sala, wakatoa kipaumbele cha pekee kwa vijana waliokuwa wanaoishi katika mazingira hatarishi, ili kuwapatia matumaini ya maisha bora zaidi. Mwenyeheri Yohane wa ishirini na tatu aliasisi Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unaoadhimisha Jubilee ya miaka hamsini katika Mwaka wa Imani, matendo makuu ya Mungu.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili ni mmissionari mahiri ndani ya Kanisa, aliyethubutu kupeleka ujumbe wa Habari Njema hadi miisho ya dunia; aliyewatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza anasema, alitamani kumtangaza Yohane Paulo wa Pili kuwa Mtakatifu hapo tarehe 8 Desemba 2013, lakini inaonekana itakuwa ni vigumu kwa waamini na watu wa kawaida kutokana na theluji kuanza kuanguka.

Tarehe nyingine elekezi pengine itakuwa ni wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme, tarehe 24 Novemba 2013 wakati wa Kufunga Mwaka wa Imani, lakini haitawezekana. Tarehe nyingine ni katika Maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, zote hizi ni tarehe elekezi lakini bado Kanisa linaendelea kuangalia tarehe muafaka.

kumbe, anasema Baba Mtakatifu kwamba, tarehe 8 Desemba, 2013, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, HATAWEZA KUTANGAZWA KUWA MTAKATIFU. Wote wawili wanatarajiwa kutangazwa siku moja kuwa ni watakatifu kwani hawa ni miamba wa imani wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu shutuma mbali mbali kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa anasema kwamba, wale walioshutumiwa, wamefanyiwa uchunguzi wa kina na hakuna ukweli wowote. Kuhusu mashoga anasema, si kazi yake kumhukumu mtu kutokana na hisia na jambo la msingi ni mtu mwenyewe kutubu na kumwongokea Mungu na daima ataweza kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake.

Mashoga wasitengewe, wasaidie kujisikia kuwa ni sehemu ya Jamii. Jambo linalosikitisha ni kuona kwamba, kuna watu wanataka kutumia hisia hizi kwa ajili ya kujijenga kisiasa.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.