Poland inaanza kufungua malango yake kwa Maadhimisho ya Siku ya 29 ya Vijana Duniani
kwa kumkumbuka Mwenyeheri Yohane Paulo II
Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland anasema,
amepokea kwa moyo mkuu ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuadhimisha Siku ya 29
ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016, Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland. Hii ni habari
ya furaha, dhamana na uwajibikaji mkubwa mbele yao. Mwaka 2016, Poland itakuwa inaadhimisha
miaka 1050 ya Uinjilishaji.
Kanisa na Serikali ya Poland, inamshukuru Baba
Mtakatifu Francisko kwa kupokea mwaliko kutoka Poland ulioonesha hamu na kiu ya vijana
wengi kutaka kuadhimisha sherehe ya imani yao nchini Poland kwa kumkumbuka kwa namna
ya pekee Mwenyeheri Yohane Paulo ambaye kunako mwaka 1978 aliondoka nchini Poland
kwa kukabidhiwa dhamana ya kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro na muasisi wa Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani.
Daima Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alikuwa na
matumaini makubwa kwa vijana katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Poland
inaanza kufungua malango yake ili kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia
sasa, iweze kuwapokea mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Poland inamshukuru
Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameonesha nia ya kutaka kutembelea Poland, mahali
alipozaliwa Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili ambaye anatarajiwa kutangazwa na Mama
Kanisa kuwa Mtakatifu hivi karibuni.