2013-07-28 08:57:30

Wizi wa dawa unatia kichefuchefu!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amewaagiza madiwani wa Halmashauri zote nchini humo kudhibiti wizi wa dawa katika hospitali na vituo vingine vya afya nchini. Aidha, Rais Kikwete amewaagiza madiwani kuanza kuweka kwenye bajeti za halmashauri zao fedha za kujengea nyumba za walimu wa shule mbalimbali nchini kama njia ya haraka ya kumaliza tatizo la uhaba wa nyumba za walimu.

Pia Rais Kikwete amesema kuwa mbali na walimu, ni wajibu wa madiwani na Halmashauri nchini kuweka katika bajeti zao fedha za kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali na shule wanazosoma ama wanaoishi katika mazingira hatarishi. Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo, Ijumaa, Julai 26, 2013, wakati alipozungumza na wananchi wa Biharamulo mjini kabla ya kuweka jiwe la msingi la Barabara ya Kagoma-Lusahunga.

Akizungumza kwenye sherehe hizo zilizofanyika nje ya Mji wa Biharamulo kwenye njia panda ya kwenda Lusahunga, Rais Kikwete amewaambia madiwani kuwabana watendaji katika halmashauri mbalimbali na kusimamia usambazaji waharaka na usiokuwa na wizi wa dawa. “Taarifa hizi za wizi wa dawa zinaudhi sana. Serikali inahakikisha kuwa inatoa dawa za kutosha lakini bado dawa hizo haziwafikii wananchi.

Wakati mwingine mtu anakwenda hospitali, anaandikiwa dawa na kuelekezwa aende kwenye duka la dawa kumbe duka lenyewe ni mali ya aliyeandika hiyo karatasi ya maelekezo ya dawa. Kuna udanganyifu mwingi na madiwani lazima watusaidie,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kuhusu uhaba huu wa nyumba za walimu ni vyema kuwa halmashauri zetu nchini kuanza kujihusisha na ujenzi huo kwa kuweka katika bajeti zao fedha za kujenga nyumba za walimu. Hawa ni walimu wako chini ya Halmashauri sasa inakuwaje halmashauri zisijihusishe na ustawi wao?”

Mapema, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli amewaasa viongozi wa Halmashauri nchini kuhakikisha kuwa wanatumia fedha nyingi ambazo wanapewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika maeneo yao lakini wanashindwa kutumia fedha hizo.

“Tunatoa fedha nyingi kutoka kwenye Road Fund lakini viongozi wa Halmashauri mbalimbali wanashindwa kuzitumia na badala yake unafika mwisho wa mwaka wa fedha wakati fedha hizo bado ziko mikononi mwao na wananchi wanaendelea kulalamikia barabara mbovu. Hizi siyo fedha zao, ni fedha za wananchi kwa ajili ya ustawi wao kwa kuwajengea barabara.”








All the contents on this site are copyrighted ©.