2013-07-28 08:41:49

Vijana kutoka Bara la Afrika waguswa na ukarimu wa wananchi wa Brazil


Wawakilishi wa vijana kutoka Barani Afrika ni kati ya bahari ya watu ambao imekuwa ikihudhuria Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro. Licha ya uchovu, mvua na pilika pilika za maadhimisho haya, vijana kutoka Barani Afrika wanasema, wameonja umoja na mshikamano katika imani, matumaini na mapendo kutoka kwa vijana wanaohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Vijana huko Rio de Janeiro.

Kwa hakika, kimekuwa ni kipindi cha kujenga na kuimarisha Umoja na Mshikamano kati ya Kanisa la kiulimwengu pamoja na Kanisa Katoliki nchini Brazil ambao ni wenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani. Vijana wengi kutoka Barani Afrika wameonja ukarimu wa waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Brazil.

Vijana wamepata fursa ya kuweza kuwashirikisha vijana wenzao: mang'amuzi ya maisha, imani, vipaumbele na matarajio yao kwa siku za usoni. Ni matumaini ya vijana kutoka Barani Afrika kwamba, changamoto wanazokumbana nazo, zitakuwa ni nyenzo kuu katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho Barani Afrika, changamoto kutoka kwa Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu Barani Afrika.

Makundi ya vijana kutoka Barani Afrika yameongozwa na Maaskofu, Mapadre na Watawa wanaojihusisha na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana. Kuna idadi kubwa ya vijana kutoka Afrika ambao wameshiriki pia katika kazi za kujitolea na huduma kwa vijana wenzao, hali inayoonesha umuhimu wa huduma ya mapendo kwa jamii.

Vijana wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, matumaini ambayo yanapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, ambaye hadanganyi wala kudanganyika! Huu ni ujumbe unaopaswa kufanyiwa kazi na vijana Barani Afrika katika jitihada za kuwa ni Wamissionari miongoni mwa vijana wenzao na kwamba, wanatumwa kuwa ni wajenzi wa amani, upendo na mshikamano katika Jamii ambamo vita, kinzani na madhulumu yanazidi kutawala na kufisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Katika Maadhimisho haya, vijana hawa wamejisikia kuwa kweli ni Wamissionari miongoni mwa vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, ni uzoefu na mang'amuzi ambayo haitakuwa rahisi sana kufutika katika akili na moyo wa mtu. Vijana waliokuwa wanahudumiwa wameonesha moyo wa kujali na kuthamini sadaka iliyokuwa inatolewa na vijana wenzao kwa ajili yao.

Vijana kutoka Barani Afrika wanakiri kwamba, wameguswa kwa namna ya pekee na katekesi, liturujia na shuhuda mbali mbali zilizokuwa zinatolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro. Lakini jambo ambalo linaendelea kuwagusa watu wengi ni ukarimu wa wananchi wa Brazil. Wananchi wameonesha upendo na mshikamano kwa mahujaji waliokuwa wanahitaji msaada wa hali na mali, lakini zaidi kwa uwepo wao.

Waswahili wanasema "kwenye msafara wa mamba, kenge hawakosekani"! Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Imani kwa Vijana, hawakukosekana watu waliotaka kufanya fujo na vioja dhidi ya Serikali na Mafundisho ya Kanisa. Baadhi yao wamekuwa wakiandamana huku wamevaa "suti ya Adamu" kudai uhuru wa kutoa mimba dhidi ya mafundisho ya Kanisa. Lakini, hawa ni wachache, ikilinganishwa na umati mkubwa wa vijana na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wanashiriki matukio mbali mbali kama sehemu ya Maadhimisho ya Juma la Vijana huko Rio de Janeiro kwa Mwaka 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.