2013-07-28 07:40:38

Ujumbe wa Baba Mtakatifu katika Kesha la kufunga Siku ya 28 ya Vijana Duniani, Rio 2013


Kesha la Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 limefanyika kwenye Ufuko wa Copacabana, Rio de Janeiro, Brazil na kuhudhuriwa na bahari ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kesha hili liligawanyika katika sehemu kuu mbili, yaani Liturujia ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Vijana wamefanya onesho linaloangalisha umuhimu wa vijana kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kristo. Wahusika wakuu katika sehemu hii, walikuwa ni vijana Wafranciskani.

Vijana wametoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na baadaye wakamuuliza Baba Mtakatifu Francisko maswali kadhaa. Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Francisko wa Assis alipokuwa kwenye tafakari ya kina, alisikia sauti ya Kristo ikimwalika kumjengea Kanisa, yaani kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya huduma makini. Hata leo hii, Kristo anahitaji vijana wachangamfu na wenye imani thabiti wanaoweza kujitosa kimaso maso kwa ajili ya kutangaza na kumshuhudia Kristo sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya maisha yao adili.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu anaendelea kupandikiza mbegu ya Neno lake katika moyo wa kila kijana, changamoto na mwaliko kwa kila kijana kutoa nafasi ili Neno la Mungu liweze kupata maskani katika moyo na maisha ya kijana. Neno hili likue na kukomaa, kwa kutambua kwamba, wao ni Wakristo "Full Time" na wala si Wakristo wa kipindi cha mpito, kama moto wa mabua! Ni Wakristo wa kweli na wema mbele ya Mwenyezi Mungu; wanaoishi katika uhuru wao bila ya kumezwa na malimwengu, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ni njia, ukweli na uzima.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, Yesu Kristo anawaalika kuacha yote na kumfuasa maisha yao yote ili waweze kutenda kama Jumuiya, jambo ambalo linahitaji mazoezi. Hii ndiyo changamoto pia iliyoko mbele ya wafuasi wa Kristo wanaopaswa kufanya mazoezi ili kuwa na maisha bora, yanayozaa matunda ya utakatifu wa maisha, ili hatimaye, waweze kupata maisha ya uzima wa milele.

Ili kufanikisha changamoto hii, kuna haja ya kujenga na kuimarisha majadiliano ya kina na Yesu Kristo kwa njia ya: Sala ambayo ni majadiliano ya kila siku na Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu, daima anawasikiliza; Ushiriki mkamilifu wa Sakramenti unawawezesha kuonja uwepo wa Mungu kadiri ya mapenzi ya Yesu; kwa njia ya upendo wa kidugu, wataweza kusikilizana, kufahamiana, kusameheana, kupokeana na kusaidiana bila kuwatenga wala kuwasukumiza wengine pembezoni.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, mioyo yao ni udongo mzuri ambao unaweza kupokea Neno la Mungu, hata pale wanapopambana kulimwilisha Neno hili katika uhalisia wa maisha yao, watambue kwamba, wao ni sehemu ya Familia inayofanya hija hii ya maisha; wao ni sehemu ya Kanisa na kwamba, wanachangamotishwa kuwa ni wadau na wajenzi wa Kanisa na historia kwa ujumla. Vijana ni mawe hai katika ujenzi wa Kanisa hai la Yesu linaloweza kuwakumbatia watu wote. Kanisa halina budi kuwa ni kwa wote.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha tafakari yake katika Kesha la Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa kuwakumbusha kwamba, Yesu bado anamwambia kila mmoja wao, kwamba, "Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi." Mama Teheresa wa Calcutta anasema, mchakato huu wa mabadiliko ndani ya Kanisa unaanza kwako na kwangu pia!







All the contents on this site are copyrighted ©.