2013-07-28 07:44:21

Papa na changamoto za Kanisa Katoliki nchini Brazil!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 amekutana na kuzungumza na Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu kutoka Brazil wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbusha Makleri wa Brazil kwamba, Mkutano wa Aparecida ni ufunguo wa maisha na utume wa Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini.

Watu wana njaa na kiu ya kupata mahitaji yao msingi kwa kuvunja kuta za utengano na ubaguzi, kwani Mwenyezi Mungu anapania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa halina budi kujifunza subira na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ni jambo la ajabu kwamba, Mwenyezi Mungu anapata nafasi zaidi katika maisha ya watu maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, Kanisa linatumwa kumuundia Mwenyezi Mungu mazingira ili aweze kukutana na kuzungumza na watu wake.

Mama Kanisa amekabidhiwa utume wa kimissionari ambao unapaswa kutekelezwa kwa ari na moyo wa unyenyekevu kwani Mwenyezi Mungu anataka kujifunua kwa Kanisa kwa njia ya maskini na wanyonge, kwa kutambua kwamba, mikakati na utekelezaji wa shughuli za kichungaji haiwezi kujitosheleza kwa kujikita katika utajiri na rasilimali iliyopo, bali katika kipaji cha ugunduzi wa upendo na kwamba, Kanisa linatumwa kushusha nyavu zake tena na tena kwa ajili ya ukombozi wa binadamu. Kanisa Katoliki nchini Brazil haliwezi kusahau utume unaojikita katika maisha ya watu wake.

Baba Mtakatifu amelipongeza Kanisa nchini Brazil katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Kutoka katika Majimbo 12 yaliyokuwepo wakati wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hadi kufikia Majimbo 275 kwa sasa. Hizi ni juhudi, ari na moyo wa Maaskofu na Wamissionari waliojitosa kimaso maso kwa ajili ya kuwatangazia wananchi wa Brazil Habari Njema ya Wokovu, changamoto ya kuonesha upendo wa pekee kwa waamini ambao wamekabidhiwa na Mama Kanisa ili kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza.

Viongozi wakuu wa Kanisa daima wamekuwa bega kwa bega na Kanisa nchini Brazil tangu nyakati za uongozi wa Mwenyeheri Yohane wa Ishirini na tatu, aliyekazia umuhimu wa kuwa na mikakati makini ya shughuli za kichungaji; Mtumishi wa Mungu Paulo wa sita aliyehimiza Kanisa nchini Brazil kuwa aminifu kwa Kristo pamoja na kupokea changamoto zilizokuwa zimetolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, pamoja na kujikita katika azma ya Uinjilishaji.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ameendelea kukazia kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini Brazil kwa kuhimiza: umoja na ushirikishwaji sanjari na maandalizi makini ya Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Mkutano mkuu wa tano uliomshirikisha Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, umeweka dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Jambo la msingi ambalo Maaskofu wanapaswa kuendelea kujiuliza ni kitu gani ambacho Mwenyezi Mungu anataka kutoka kwao wakati huu?

Baba Mtakatifu anasema, hija ya wafuasi wa Emmaus baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni mfano mzuri wa kujifunza kwa kuangalia mapungufu na changamoto zilizopo kwa sasa, kwa kuangalia ukuaji wa mtu hatua kwa hatua; watu ambao wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kiimani, kiasi kwamba, leo hii ni watu ambao wamemweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa maisha yao: kwa maneno na matendo. Hapa kunahitajika Kanisa linalojikita katika toba na wongofu wa ndani, Kanisa lenye uwezo wa kujadiliana na watu katika maisha na utume wake, ili kuweza kuzima kiu na njaa ya watu katika maisha yao ya kiroho.

Ulimwengu wa utandawazi na ukuaji wa miji unatoa ahadi nyingi kwa mwanadamu wa leo, lakini kwa bahati mbaya ahadi hizi zimekuwa ni sawa na ndoto. Watu wanajikuta wakikabiliana uso kwa uso na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu; ongezeko la familia tenge; watu wamepoteza maana ya maisha; hawana utambulisho tena; wanagubikwa na upweke hasi, unaotishia maisha na ustawi wao kama binadamu.

Kuna kinzani, migawanyiko na migongano ya kijamii. Watu wamepoteza fadhila ya kupenda, kusamehe, kusahau, kufahamu, hali inayosababisha machungu ya ndani na kuyafanya maisha kukosa utamu. Matokeo yake, watu wanakimbilia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia, ngono na wengi wao wametafuta njia za mkato kwani Mafundisho, Taratibu na Kanuni na Maisha ya Kanisa ni magumu mno!

Leo hii kuna haja ya kuwa na Kanisa linalowasindikiza watu kwenda mbali zaidi na Kusikiliza, Kanisa linalofanya hija na waamini; Kanisa linalotambua sababu za watoto wake wengi kulikimbia na kutafuta malisho sehemu nyingine! Kanisa ambalo lina uwezo na ujasiri wa kupasha joto mioyo ya watu na kuwasindikiza watu kuelekea Yerusalem mpya na nyumbani kwa Baba.

Baba Mtakatifu anasema, leo hii mambo yanayokwenda kwa haraka yana mvuto na mashiko! Hali hii inaonesha kwamba, watu wanakosa amani na utulivu wa ndani. Je, Kanisa liko tayari kutembea taratibu kwa kuwasikiliza watu kwa umakini mkubwa na uvumilivu unaowawezesha waamini kujisikia kuwa wako nyumbani, wanapendwa na kuthaminiwa.

Baba Mtakatifu anasema, changamoto kubwa zinazolikabili Kanisa Katoliki nchini Brazil zinaweza kufanyiwa kazi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa majiundo makini ya viongozi wa Kanisa wanaoweza kutembea katika usiku wa giza bila kuvamiwa na hatimaye kupotelea huko gizani; watu wenye uwezo wa kusikiliza bila kushawishika; wanaoweza kuwapokea wengine bila kujutia vitendo vyao; viongozi ambao ni makini na wanaoonesha utambulisho wao. Ni watu waliofundwa kikamilifu katika utu wema na maisha adili; utamaduni na maisha ya kiroho; watu wanaofahamu vyema Mafundisho ya Kanisa.

Kanisa Katoliki Brazil anasema Baba Mtakatifu halihitaji kiongozi mwenye karama, bali mnyororo wa mshikamano wa viongozi wa Kanisa unaoonesha ushuhuda wa umoja katika maneno na matendo; watu ambao wanaweza kupokea na kukubali tofauti, wote kwa pamoja wakishirikishana mang'amuzi na uhusiano wao na Yesu Kristo Mfufuka. Ni mshikamano unaofanywa na Maaskofu mahalia katika Majimbo yao na Kanisa zima nchini Brazil. Ni mshikamano unaojikita katika umoja kama utajiri mkubwa wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kuna haja ya kukazia maisha na utume wa Kanisa unaojikita katika toba na wongofu wa shughuli za kichungaji, kielelezo makini cha ushuhuda wa imani. Shughuli za kichungaji ni yuekelezaji wa huduma ya kimama inayofanywa na Kanisa kwa njia ya huruma ili kuponya madonda na majereha ya binadamu wa leo wanaohitaji kuonjeshwa huruma, upendo na kusamehewa.

Mikakati ya shughuli za kichungaji, itoe kipaumbele cha kwanza kwa familia: msingi wa maisha ya Kanisa na Jamii; vijana wanaoonesha sura ya Kanisa kwa siku za usoni; wanawake ambao wanadhamana kubwa ya kurithisha imani na kwamba, hili ni kundi lenye mchango mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia Maaskofu Katoliki Brazil kwamba, Kanisa katika utekelezaji wa mikakati yake katika Jamii, linaomba uhuru wa kutangaza Injili ya Kristo hata pale ambapo ujumbe huu unakumbana na kinzani na misigano ya kijamii. Kanisa linataka kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa lina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba, linaendelea kuwasha mshumaa wa uhuru na umoja miongoni mwa binadamu kwa kukazia: elimu makini, afya bora na amani jamii.

Haya ni mambo msingi kwa Brazil kwa nyakati hizi. Kanisa lina mchango wake kwa kila changamoto inayojitokeza nchini Brazil kwa kuwa na mwono sahihi kuhusu mwanadamu na utu wake pamoja na kumpatia Mungu nafasi katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu analishukuru Kanisa Amerika ya Kusini kwa moyo wa mshikamano na upendo kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kutoka Haiti, wanaotafuta kuboresha hali ya maisha yao baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi. Hapa kuna haja ya kulinda na kutunza mazingira ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kanisa Katoliki nchini Brazil tangu mwaka 1997 limeonesha mshikamano wa dhati kwa kutuma wamissionari mapadre, watawa na walei kwa ajili ya maeneo ya Amazonia.

Lakini hapa kuna haja ya kuwa na walezi makini walioandaliwa barabara; Majaalim wa taalimungu watakaosaidia kuimarisha matunda yaliyokwishakupatikana katika malezi, pamoja na kuwa na Makleri wanaofahamu mazingira yao ili kuimarisha sura ya Kanisa mahalia. Huu ndio ujumbe makini ambao Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwashirikisha Makardinali na Maaskofu Katoliki nchini Brazil.







All the contents on this site are copyrighted ©.