2013-07-28 11:04:24

Baba Mtakatifu ameonesha changamoto na vipambele kwa Kanisa katika ulimwengu mamboleo!


Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Jumamosi, tarehe 27 Julai 2013, kabla ya Baba Mtakatifu Francisko hajaanza kujimwaga kwa moyo na akili zake zote kwa ajili ya Mkesha wa Maashimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil na Amerika ya Kusini katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu amezungumza na Maaskofu hao kwa takribani dakika arobaini na tano, akionesha vipaumbele vya maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji ambavyo Kanisa linapaswa kuvifanyia kazi katika azma ya Uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu amefanya rejea kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Amerika ya Kusini uliofanyika mjini Aparecida kunako mwaka 2007 na kufunguliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Wakati huo Kardinali Bergoglio, akiwa Kardinali na Askofu mkuu kutoka Argentina, alishiriki kwa ukamilifu na kwamba, ni mtu anayefahamu kwa kina na mapana undani wa Waraka uliotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini. Tafakari yake wakati huu, ni mwaliko na changamoto kwa Kanisa Amerika ya Kusini kuimwilisha katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anapenda pia kuwachia ujumbe wajumbe wa Sekretarieti ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, kabla ya kufunga vilago katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Ni ujumbe ambao unajikita katika mwelekeo, vipaumbele, tasaufi na mikakati ya Kanisa katika mchakato wa kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu akiwa mjini Rio de Janeiro amezungumza na viongozi wa Serikali, Wanasiasa, Wachumi na Wawakilishi wa makundi ya watu mbali mbali nchini Brazil. Kijana mwenye umri wa miaka 28 ambaye amepitia shida na mahangaiko ya baa la umaskini, matumizi haramu ya dawa za kulevya na hatimaye akagundua kwamba yote hayo yalikuwa ni ubatili mtupu na furaha ya mpito iliyomwachia ukakasi wa maisha!

Akaacha yote na kuanza kusoma, leo hii ni Jaalim na mwamini anayeshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, huyu ndiye aliyepewa fursa ya kuzungumza kwa niaba ya wasomi wa Brazil mbele ya Baba Mtakatifu Francisko. Ni kijana aliyeonesha ukomavu na matumaini makubwa, changamoto ambayo pia imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anazungumza na wasomi kutoka Brazil, kwa kukazia ujenzi wa utamaduni wa kukutana, ili kuanzisha mchakato wa majadiliano kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi.

Baba Mtakatifu amezungumzia siasa kuwa ni kama Jukwaa la hali ya juu la huduma ya upendo kwa jirani. Hii ni huduma inayopaswa kuwashirikisha watu wengi zaidi.

Padre Federico Lombardi anasema, Baba Mtakatifu amefuatilia kwa umakini mkubwa Ibada ya Njia ya Msalaba na Tafakari yake na kuona jinsi ambavyo inajikita katika uhalisia wa maisha ya vijana wengi leo hii. Ni tafakari iliyokuwa na maneno machache na mafupi, lakini ilikuwa inaacha chapa ya kudumu katika moyo wa mtu!

Kimsingi tafakari hii imegusia mahitaji msingi ya vijana, ukosefu wa fursa za ajira, mateso na mahangaiko ya vijana kutokana na magonjwa; nyanyaso na hali ya kutengwa; wanawake na changamoto za maisha, watu wanaojitolea ili kuwaonjesha wengine tone la upendo, yote haya yaliunganishwa ili kuonesha mshikamano wa upendo na Kristo Msulubiwa, aliyeukirimia ulimwengu wokovu pamoja na kuwaonjesha walimwengu upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Njia ya Msalaba imekuwa ni kivutio kikubwa kwa tafakari ya vijana ili kugundua matukio mbali mbali ya maisha ya ujana na changamoto zake.







All the contents on this site are copyrighted ©.