2013-07-27 09:05:20

Yaliyojiri siku ya Ijumaa!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko siku ya Ijumaa asubuhi kwenye kitongoji cha Quinta de Boa amewaungamisha vijana watano kwenye hema lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya maungamo kwa vijana.

Watawa wa Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta, waliwasindikiza vijana waliokuwa wanaungama kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Hawa ni vijana waliochaguliwa kwa bahati nasibu. Baba Mtakatifu alisali kwa ukimya na baadaye akaanza kuungamisha kadiri ya Mapokeo ya Kanisa. Ametumia dakika 25 kuwaonjesha vijana hawa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Vijana wengi wametumia siku hii kwa ajili ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Baba Mtakatifu Ijumaa mchana alipata pia fursa ya kuzungumza na vijana sita waliokuwa wanatumikia kifungo gerezani. Amezungumza pia na viongozi wa Kanisa na Gereza waliokuwa wamewasindikiza vijana hawa. Viongozi wa gereza wamemshukuru Baba Mtakatifu na Kanisa kwa ujumla kutokana na huduma makini wanayotoa kwa ajili ya wafungwa magerezani: kiroho na kimwili.

Vijana hao wamemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko hali na magumu wanayokabiliana nayo gerezani; wamempatia barua kutoka kwa wafungwa kwa niaba ya wafungwa wenzao. Kimsingi wamemshukuru na kuahidi kuendelea kumwombea Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake. Wamemzawadia Baba Mtakatifu Rozari waliyoitengeneza wakiwa gerezani, huku wakionesha majina ya vijana waliouwawa kikatili nchini Brazil, takribani miaka 20 iliyopita.

Baba Mtakatifu amesema hakuna haja ya kufanya vurugu, bali kumwilisha upendo. Kwa pamoja waliweza kusali kwa ajili ya kuwaombea vijana hao na Baba Mtakatifu amewaalika waendelee kusali pia kwa ajili ya maisha na utume wake. Padre Federico Lombardi anasema huu ndio mwelekeo wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, si tu kwa wale wanaobahatika kufika, bali vijana wote walioenea sehemu mbali mbali za dunia, katika raha, shida na mahangaiko yao ya ndani.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa chakula cha mchana, aliwaona vijana wakiwa na wasi wasi, akawauliza mbona mna wasi wasi hivi, wao wakasema, kwa mara ya kwanza katika maisha ya ujana wao wamebahatika kula pamoja na Baba Mtakatifu. Baba Mtakatifu amezungumza na vijana hawa akiwauliza kuhusu dira na mwelekeo wa dhana ya Kanisa waliyo nayo moyoni mwao na kwamba, amewataka kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa, wajitahidi kuishi katika Jumuiya na kamwe wasigubikwe na ubinafsi, waoneshe dunia inayosimikwa katika utu na maisha ya binadamu!

Tatizo kubwa katika ulimwengu mamboleo ni vijana kugeuzwa kuwa ni vichokoo na vivutio vya masuala ya uchumi. Amewataka vijana kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuboresha maisha yao ya kiroho, pale inapowezekana kuwa na Mlezi wa maisha ya kiroho, anayeweza kumsindikiza katika safari yake ya ndani, huku wakiendelea kuwaonjesha wengine upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, aliyewapenda upeo.

Baba Mtakatifu anawataka vijana hao kujiuliza swali la msingi juu ya uwepo wao kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani; Kwa nini kuna mateso na mahangaiko mengi duniani? Mbona watu wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na baa la njaa wakati dunia inaweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa watu wengi zaidi?

Baada ya sala, Baba Mtakatifu amewapatia zawadi kama kumbu kumbu ya mlo wao wa pamoja! Vijana wanasema, kamwe, hawataweza kusahau tukio hili katika maisha yao! Kujichana na Baba Mtakatifu, kwa hakika si haba!







All the contents on this site are copyrighted ©.