2013-07-27 15:04:21

Makleri na Watawa wanachangamotishwa kuwa ni wahudumu wa umoja na utamaduni wa kukutana wakiongozwa na ukweli kuhusu Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 27 Julai 2013, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani, amekutana na kusali pamoja na Makleri, Waseminari na Watawa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Sebastiani, Rio de Janeiro.

Baba Mtakatifu anasema, lengo la Maadhimisho ya Ibada hii ya Misa takatifu ni kwa ajili ya kumsifu, kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu, kwani wameitwa na hatimaye, wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na ujenzi wa utamaduni wa majadiliano. Kwa njia hii wataweza kuishi, kutenda na kupata ufanisi katika huduma na utume wao, ikiwa kama Kristo atakuwa anaishi ndani mwao, mwaliko wa kuendelea kujishikamanisha na Kristo katika huduma kwa maskini na wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; sala na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu anawaambia Makleri na Watawa kwamba, wanatumwa kutangaza Injili ya Kristo, mwaliko wa kuwasaidia vijana kutambua kwamba, wanaitwa kuwa ni Wafuasi na wanatumwa kama Wamissionari wa Yesu kuinjilisha kwa kuanzia katika familia zao, maeneo ya masomo na kazi, ndugu, jamaa na marafiki. Ni mwaliko wa kuwaendea wale walioko pembezoni mwa Jamii, wanaojisikia pweke na wale ambao kwa miaka mingi hawajauona mlango wa Kanisa, wao pia wanaalikwa kushiriki Karamu ya Bwana.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kama Makleri na Watawa wanalikwa kuwa ni wajenzi wa utamaduni wa majadiliano na maelewano dhidi ya utamaduni mamboleo unaojikita katika hali ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; ni ulimwengu ambamo wazee hawana nafasi tena na watu wanakumbatia utamaduni wa kifo; ni utamaduni unaowafanya watu kutokuwa hata na muda wa kubadilishana mawazo na jirani zao, kwani daima wako katika haraka na pilika pilika za maisha; hapa mahusiano yanajengeka katika tija na ufanisi wa mtu.

Makleri na Watawa wawe na ujasiri wa kubadili mwelekeo kwa kukazia umuhimu wa familia kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; kwa kuonesha moyo wa ukarimu, mshikamano, upendo na udugu; tunu msingi zinazowezesha maisha ya binadamu kujikita katika utu. Kama viongozi wa Kanisa, anasema Baba Mtakatifu wanapaswa kutambua kwamba, ni wahudumu wa umoja na utamaduni wa kukutana, huku wakiongozwa na fadhila ya unyenyekevu inayofumbatwa katika ukweli wa kukutana kwanza na Yesu Kristo.

Askofu mkuu Oran Joao Tempesta wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro, akizungumza kwa niaba ya Makleri, Watawa na Waseminari, amesema wanachangamotishwa na Kanisa Amerika ya Kusini kuwa ni Walimu na Wanafunzi, ili kuweza kumsikiliza Khalifa wa Mtakatifu Petro anayewashirikisha mang'amuzi ya maisha kwa ajili ya utekelezaji wa utume ambao wamekabidhiwa na Mama Kanisa.

Kama viongozi wa Kanisa wanachangamotishwa kwenda duniani kote ili kuwafanya mataifa yote kuwa ni wanafunzi, changamoto ambayo imechukua mwelekeo wa pekee kunako mwaka 2007 na kwa wakati huu katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Kanisa Katoliki nchini Brazil linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani; wanamwomba ili azidi kuwaimarisha katika mwanga wa imani pamoja na kuwabariki katika huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika: haki, amani, udugu na matumaini.







All the contents on this site are copyrighted ©.