Rais Jakaya Mrisho ameamuru majambazi na wahamiaji haramu wote katika mikoa mitatu
nchini kujisalimisha katika muda wa siku 14 kuanzia Ijumaa, Julai 26, 2013 kabla ya
kuanza kwa operesheni kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania nyenye lengo la
kukomesha ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.
Rais Kikwete
ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa leo ametoa amri kwa vyombo vyote vya ulinzi
na usalama nchini kuanza maandalizii ya operesheni hiyo na hatimaye kuiendesha katika
Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. “Majambazi wanateka magari, wanaua watu wetu, wanapora
mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu katika nchi
yao wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani, tutachimbua ardhini
kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete
ametoa amri hiyo, Ijumaa, Julai 26, 2013 wakati alipohutubia wananchi wa mjini Biharamulo,
Mkoani Kagera, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya lami kutoka
Kagoma, Wilaya ya Muleba kwenda Lusahuga, Biharamulo. Rais Kikwete ametoa amri hiyo
kufuatia matukio ya mara kwa mara na yasiyokuwa na mwisho ya majambazi kuteka mabasi,
kuua watu na kupora mali zadi katika mikoa hiyo, hali ambayo imesababisha malalamiko
ya wakazi wa mikoa hiyo.
Rais Kikwete ameaambia wananchi: “Tumeamua kukomesha
upuuzi huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma Geita. Leo nimetoa maagizo kwa vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Usalama wa
Taifa kuandaa operesheni maalum, operesheni kubwa kuliko zote tokea tupate uhuru.
Upuuzi huu hauwezi kuendelea.”
Ameongeza Rais Kikwete na kuwaambia wananchi:
“Nawaamuru majambazi wote, wenye kumiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu
wote wajisalimishe katika wiki mbili kuanzia leo. Wajisalimishe wao pamoja na silaha
zao. Baada ya hapo, tunaanzisha operesheni ambayo haijapata kuonekana katika historia
ya nchi yetu.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Sitanii, sina mzaha na hili. Nimechoka.
Nalisema hili mchana, macho makavu. Nawaambia majambazi watafute kazi nyingine, kazi
hii hailipi tena. Kwa wale majambazi na wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani, waanze
safari ya kurejea kwao.” Rais Kikwete ameonya: “Na hata wale wanaoishi na kulea majambazi
na wahamiaji haramu nao wajisalimishe. Na ole wao majambazi watakaojaribu kuwapiga
risasi askari wetu. Watakiona cha mtema kuni.”