2013-07-27 14:33:08

Maadhimisho ya Juma la Vijana na ukuaji wa miito nchini Tanzania


Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Yakobo Mtume, sanjari na Maadhimisho ya Juma la Vijana, ambamo Mama Kanisa anawaalika kwenda ulimwenguni kote kuwafanya mataifa kuwa ni wanafunzi wa Kristo, Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, iliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapongeza Majandokasisi walipiga hatua mbali mbali katika majiundo yao ya kikasisi. Yafuatayo ni mahubiri ya Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania.

Ndugu zangu; tumekusanyika hapa katika adhimisho la SADAKA TAKATIFU YA MISA kuwapongeza na kuwasindikiza katika safari yao ya wito ndugu zetu MAFRATERI GODFREY BOGE, ALOIS MAZENGO, HILLARY NGOWI, BARAKA JINGU, FAUSTINE MAGANGA, SEBASTIAN MBEGANI, BONAVENTURE MUSHI NA SEVERINE ANGELUS. Hawa wamemaliza mwaka wa pili wa malezi katika nyumba yetu ya Malezi ya Mtumishi wa Mungu Yohane Merlini – MIYUJI – DODOMA na wanajiandaa kuanza masomo ya Taalilimungu katika chuo cha JUCO. Wanapewa mavazi rasmi ya kifrateri. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya wito aliyowajalia ndugu zetu hawa.

Maisha ya wito – maana yake ni maisha ya kumfuata Mungu na ni itikio la mtu katika uhuru wake akimfuata Roho wa Mungu na akitaka kutimiza mapenzi ya Mungu Baba. Historia ya kanisa inaongozwa na Mungu mwenyewe anayemwita mwanadamu na kumtuma aende akafanye kazi aliyomwagiza. Yafaa nini mtu kuupata ulimwengu wote na kuiangamiza nafsi yake? Matayo 19,16. Kila mmoja wetu anatambua jinsi ilivyo vigumu kuondokana na mazoea yetu, hali tulizozea, mila na desturi zetu, hali zetu, mavazi yetu tuliyozoea n.k. Uamuzi wenu huu unatoa majibu juu ya uwezekano wa kufanya tofauti katika ulimwengu huu. Lakini si kufanya tofauti tu kwa sababu ya kufanya tofauti – tofauti mnayotaka kuonesha leo hii ni katika kumtumikia Mungu kwa ushuhuda wenu wa maisha.

Katika imani, zawadi ya Mungu, tunatambua upendo mkubwa kabisa wa Mungu kwa njia ya mwanae, Yesu Kristo, Roho Mtakatifu ambaye hututakatifuza, huangazia maisha yetu yajayo na hutujalia nafasi ya kuwa wapya tukiwa na matumaini na tukiwa na furaha. No. 7 – MWANGA WA IMANI.

Imani hufungua njia ya matembezi na kutuongoza katika histori ya maisha yetu. Na ili kuweza kuelewa imani ni nini, hatuna budi kuhadithia ule mzunguko wake, njia ya wanadamu waamini, kama tunavyoona katika Agano la Kale. Kwa namna ya pekee tunamwona Abrahamu, baba yetu wa imani. Anapewa jukumu maalumu. Mungu anamwita, anajifunua kama Mungu anayeongea naye na anayemwita kwa jina. Imani huendana na kusikiliza/kusikia.

Abrahamu hakumwona Mungu, lakini anasikia sauti yake. Kwa njia hii, imani huchukua nafasi/tabia/hali ya nafsi ya mwanadamu. Hivyo Mungu huyo hafungwi na wakati, nafasi, mahali n.k bali huhusianishwa na mtu, Mungu wa Abrahamu, Isaka, Yakobo na anafanya agano na mtu. Imani huwa ni jibu kwa Neno hilo la Mungu kwake yeye anayeongea nasi. Na. 8 – Mwanga wa Imani.

Ninyi pia leo mnaingia katika mzunguko huo wa mpango wa Mungu wa ukombozi. Vueni utu wa kale – vaeni utu mpya – Efe. 4:22.... Mtakatifu Gaspar alivaa kanzu la kifrateri akiwa na miaka 10. Cfr. St. Gaspar, saint of the People – pg. 16.... tunaambiwa kuwa alitambua fika maana ya vazi lile. Alihakikisha daima linabaki safi na jeupe na mama yake anasema kwa tabasamu – kwa kanzu lako hili mwanangu umeniongezea kazi ya kuosha nguo. Alionekana nadhifu katika vazi lake hili na watu walimwita Mtakatifu mdogo na wengine walisema huyu ni mtakatifu Lui mwingine.

Mababu wa kale wanaeleza tendo la kuvaa nguo mpya kama alama ya unyofu na unyenyekevu, tendo la kuweka kando unyonge wa nguo zao za kidunia, na kuwa tayari kumvaa Mungu mwenyewe na kwa utakatifu wa maisha yao watambulike mbele ya watu kuwa wamewekwa wakfu ili kumtumikia Mungu. Wito wa Elisha – tunasikia habari juu ya maisha mapya ya Elisha. Anapotupia vazi la kinabii na nabii Eliya, anaacha yote na maisha yake yanabadilika. 1 Fal. 19: 16 – 21.


Sijui wanamitindo wetu wa wakati wa sasa watasema nini kuhusu mtazamo huu. Twafahamu wazi kuwa wao hutumika na kupitia kwao nguo zinapata jina, umaarufu, soko n.k. na baadaye mwenye bidhaa hizo anapata utajiri wa mali na fedha. Wanatumika kama watu wa mshahara, vitendea kazi tu na baadaye wao wanazeeka na kupoteza hata ile nafasi ya kutumika kama kitendea kazi.

Mavazi haya mnayopewa leo si hivyo. Ninyi si vitendea kazi bali mnapaswa kuwa watenda kazi. Mnapewa vitendea kazi. Waitaliano wana msemo – vazi halimfanyi mtu mtawa. Isiwe hivyo katika maisha yenu. Tukumbushwe tena leo na Mwinjili Lk. 12,33 – akituasa - ‘viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo kuharibu’.

Mtakatifu Fransisko wa Asissi ....alipoamua kumtumikia Mungu, alivua mavazi yake mbele ya Askofu na baba yake mzazi na kuwa tayari kuvaa mavazi kuu kuu.

Katika makabila yetu – tunakumbuka kuwa lilipowaliwa vazi fulani, pia ilimaanisha kitu/tukio/alama fulani n.k – kwa ajili ya shughuli fulani mfano mfalme, wanandoa, mashujaa, maaskari, wacheza ngoma, waombolezaji, wanawali, marehemu (maiti) n.k. Basi nanyi mtambulike na watu na wakati wote kuwa wafuasi wake Kristo kwa vazi lenu hili.



Kumbukeni daima kuwa Kristo ndiye chanzo na ukamilifu wa maisha yetu ya imani (autore e perfezionatore di nostra fede) – Ebr. 12,2 – tumkazie macho Yesu, maana ni yeye aliyeanzisha imani yetu, naye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha ya baadaye, aliustahili msalaba, asiiangalie aibu yake, naye amekaa kulia kwa kiti cha enzi cha Mungu.

Ninawaalika mpeleke imani, mapendo, na matumaini mapya katika ulimwengu na zaidi kwa vijana na watoto.
1Kor. 7,17; ‘lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo…..’. Hicho ndicho Bwana alichowagawia ninyi (kumfuata yeye katika maisha ya kitawa/kimisionari) basi na mwenende hivyo, msirudi nyuma.


Nami nawaalika ninyi na sisi wote hapa tumfuate Bwana. Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.