Familia ni mahali muafaka pa kurithisha imani, matumaini na mapendo!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 26 Julai 2013 ameianza siku kwa Ibada ya Misa
takatifu, baadaye akajiunga na Makleri wengine waliokuwa wanaungamisha vijana, tayari
kujipatia rehema na neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho haya. Baba
Mtakatifu akiwa kwenye Makao makuu ya Jimbo kuu la Rio de Janeiro amekutana na kuzungumza
na baadhi ya vijana wanaotumikia vifungo kwenye magereza ya Rio de Janeiro.
Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa mlo wa mchana amejumuika na vijana kumi na wawili ambao
ni wawakilishi wa vijana kutoka mabara matano na vijana wawili kutoka Brazil wamepata
nafasi ya upendeleo kwa kuwa ni wenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2013.
Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Kumbu kumbu ya Watakatifu
Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, Baba Mtakatifu akiwa kwenye Makao makuu
ya Jimbo kuu la Rio de Janeiro amewashukuru waamini kwa mapokezi na ukarimu mkubwa
waliomwonesha kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu
Francisko kwamba, uwepo wake mjini Rio utaamsha ari, moyo na upendo kwa Kristo na
Kanisa lake; wakionesha furaha ya kuungana na kuwa ni sehemu ya Kanisa, sanjari na
kutambua wajibu na dhamana ya kuishi na kushuhudia imani.
Baba Mtakatifu anasema
katika Familia ya Watakatifu Joakim na Anna, Bikira Maria alijifunza kusikiliza na
hatimaye, kumwilisha mapenzi ya Mungu katika hija ya maisha yake. Watakatifu hawa
wamechangia kwa kiasi kikubwa mnyororo uliowaonjesha upendo wa Mungu mintarafu dhamana
ya familia hadi kufikia kwa Bikira Maria, aliyempokea Neno wa Mungu na kumtoa kama
zawadi kubwa kwa ulimwengu. Tukio hili linaonesha umuhimu wa Familia kama sehemu maalum
kwa ajili ya kurithisha imani.
Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba,
nchini Brazil na Amerika ya Kusini kwa ujumla, Siku kuu ya Watakatifu Joakim na Anna
ni Siku kuu ya Mabibi na Mababu. Kundi hili ni muhimu sana katika Jamii kwani wana
dhamana ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kiimani, kiutu na kijamii kwa Jamii
inayowazunguka. Kumbe, kuna haja kwa vijana wa kizazi kipya kukutana na kudumisha
majadiliano kati yao na wazee hususan ndani ya familia.
Baba Mtakatifu Francisko
anahitimisha tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwa kukumbusha kwamba,
watoto na wazee ni hazina ya jamii; watoto kwa wakati muafaka, watabeba historia ya
Jamii zao na wazee wana jukumu la kurithisha uzoefu na mang'amuzi ya maisha.
Vijana
wanaohudhuria Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani wanapenda kuwasalimia Bibi
na Babu zao, waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anawashukuru
na kuwapongeza kwa ushuhuda na hekima wanayoendelea kutoa kwa vijana wa kizazi kipya
hadi sasa.