2013-07-26 08:33:38

Vijana wameitikia wito na ukarimu wa Yesu, wanataka kujenga na kuimarisha imani na urafiki wao kwa Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi jioni, tarehe 25 Julai 2013 kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani aliupokea rasmi umati wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana huko Rio de Janeiro. Tukio hili lilifunguliwa kwa onesho la sanaa ambalo, vijana walionesha hali halisi ya maisha yao ya kila siku, baadaye ilifuata Liturujia ya Neno la Mungu, wakiongozwa na kauli mbiu "Bwana ni vizuri sisi kuwapo hapa".

Baba Mtakatifu katika tafakari yake amewaambia vijana kwamba, ana matumaini makubwa na vijana na anawatakia hija njema katika maisha yao ya ujana, daima wakiwa waaminifu kwa Kristo huku wakiendelea kukumbatia Fumbo la Msalaba. Baba Mtakatifu amewakumbuka vijana waliopoteza maisha na kujeruhiwa wakati wakiwa njiani kwenda Rio de Janeiro kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Amewashukuru vijana kwa kuitikia wito kutoka kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ili kuja kuadhimisha siku kuu ya imani. Ni umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ukiwa na mila, desturi na tamaduni zao, lakini wote kwa pamoja wanaunganishwa na imani na hamu ya kutaka kukutana na Yesu, ili waweze kuwa ni wanafunzi wake. Kwa juma zima, mji wa Rio umekuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, hali inayoonesha jinsi ambavyo vijana wameitikia kwa ukarimu na ujasiri wito wa Yesu na wanaendelea kubaki pamoja naye ili wajenge urafiki wa kudumu.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana waliokuwa wamekusanyika kwenye ufuko wa Copacabana kwamba, hata leo hii, Yesu anamwita kila mmoja wao kuwa ni mfuasi na rafiki yake mwaminifu, ili aweze kuwa ni shahidi wa Injili. Hii ni changamoto pevu kwa kila mwamini hasa wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Vijana wamepata urithi mkubwa wa zawadi ya imani kutoka katika familia na jumuiya zao za Kikristo. Uwepo wake nchini Brazil unapania kuwaimarisha katika imani na ari ya kuwa ni wafuasi wa Kristo.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwasalimia na kuwatakia kheri na baraka vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaposhiriki katika Siku kuu ya Imani; wakiwa wameungana kwa pamoja, hali inayoonesha urafiki na imani pamoja na kutambua kwamba, wote hawa anapenda kuwakumbatia kama Mchungaji mkuu wa Kanisa, huku wakipokelewa na kubarikiwa na Yesu Kristo Mfalme.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wadau mbali mbali waliojitaabisha ili kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani yanapata mafanikio makubwa. Haya ni maandalizi yaliyotekelezwa tangu vijana walipokuwa Majimboni mwao. Anawashukuru wakuu wa Serikali na Kanisa waliochangia kwa hali na mali katika kufanikisha Maadhimisho haya ambayo ni kielelezo cha umoja, imani na udugu. Na kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Francissko alikuwa anafungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.

Katika hotuba yake, Askofu mkuu Oran Joao Tempesta wa Jimbo kuu la Rio, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko na bahari ya vijana iliyokuwa imekusanyika kwenye ufuko wa Copacabana kuadhimisha Mafumbo ya Imani, huku wakionesha furaha ya ujana wao na ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni tukio ambalo linafuatiliwa na umati mkubwa wa vijana kwa njia ya vyombo vya upashanaji habari, kwa sala na sadaka yao.

Uwepo wa Baba Mtakatifu ni kielelezo cha umoja wa kimissionari unaoimarisha hija ya pamoja inayofanywa na wafuasi wa Kristo wanaoandamana kwenda nyumbani kwa Baba. Hiki ni kipindi ambacho vijana wengi wamegundua na kuonja fadhila ya matumaini ndani mwao.

Vijana kutoka katika nchi 180 wamewakilishwa, kama kielelezo cha ndoto ya vijana duniani. Kuna umati mkubwa wa vijana ambao umekata tamaa kutokana na kumezwa mno na malimwengu, ubinafsi, ukosefu wa haki na usawa katika Jamii na wakati mwingine wamejikuta wakitumbukia katika furaha ya muda ambayo imegeuka kuwa ni kilio!

Askofu mkuu Tempesta anasema vijana wanazungukwa na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao, kwa njia ya imani wanapenda kukabiliana na changamoto za maisha, ili Kristo aweze kufahamika na kupendwa zaidi katika medani mbali mbali za maisha; kila kijana katika hija yake aungame imani inayomwilishwa katika utume.

Wawakilishi wa Vijana kutoka katika Mabara matano, wamemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko, ndani mwao wakiwa wamewabeba na kuwakumbatia ndugu zao katika imani, waliomwilisha Injili na wanaoendelea kuitolea ushuhuda sehemu mbali mbali za dunia. Kwa vijana kutoka Asia, wanasema, wanawakumbatia ndugu zao katika Kristo ambao wameendelea kutangaza Injili na kuishuhudia kwa njia ya majadiliano ya kidini na kiekumene.

Mwakilishi wa vijana kutoka Barani Afrika anasema, vijana wanapenda kumkaribisha kwa moyo mkunjufu huku wakisukumwa na ari na moyo wa kimissionari, licha ya magumu na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo. Vijana kutoka Oceania wanasema, umbali si kikwazo kwa wafuasi wa Kristo katika mchakato wa kudumisha umoja na udugu, kwani wanatambua kwamba, wote ni ndugu katika Kristo.

Vijana kutoka Amerika na kwa namna ya pekee wale wa Brazil wamemwambia Baba Mtakatifu kwamba, inapendeza wao kukaa pamoja. Hii ni zawadi kubwa ambayo wangependa kumkirimia, huku wakimwonesha furaha, umoja na sala zao.










All the contents on this site are copyrighted ©.