2013-07-26 11:18:58

Neno la Mungu si keki inayoliwa katika matukio maalum, bali ni chakula cha kila siku!


Askofu Michael Msonganzila wa jimbo Katoliki Musoma, Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha na majiundo ya waamini na kwamba, Neno la Mungu ni sehemu ya Imani ya Kanisa na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni Neno la Mungu na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. RealAudioMP3

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni fursa kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kulitafakari, kusali na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wasali na kulitafakari Neno la Mungu kadiri ya mazingi ra yao. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, watu wengi wametekwa na malimwengu kama vile: pilika pilika za maisha, disco, luninga, mahusiano yanayooneshwa kwenye vyombo vya habari, kiasi kwamba, hawana nafasi ya kuweza kulitafakari, kusali na kumwilisha Neno la Mungu, ambalo kimsingi ni kiungo kikuu katika maisha ya mwanadamu.

Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wao ni wadau wakuu wa utume wa Biblia, kumbe wanapaswa kujibidisha kulifahamu Neno la Mungu, wakianzia kwenye Familia, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo na katika matukio mbali mbali ya Kanisa. Neno la Mungu si keki inayoliwa wakati wa matukio maalum, bali ni chakula cha kila siku! Kwa njia hii waamini wanaweza kulitolea ushuhuda, kwani Neno la Mungu ni nguzo msingi ya imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.