2013-07-25 08:14:36

Vijana jishikamanisheni na Kristo! Kamwe hatawaangusha!


Mara tu baada ya kutembelea na kufungua Hospitali ya Mtakatifu Francisko kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya, Baba Mtakatifu aliwaalika vijana kutoka Italia waliokuwa wameunganika na vijana wenzao pamoja na Maaskofu wao kutoka Brazil na sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wakifuatilia tukio hili kwa njia ya Luninga, kusherehekea sanjari na kufanya tafakari ya kina kuhusu Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu anasema, ni Yesu Kristo peke yake anayeweza kuwapatia majibu muafaka ya imani na mahangaiko yao ya ndani. Anawaalika vijana kwa namna ya pekee, kujiachilia mikononi mwa Kristo ili aweze kuwafunda; jambo la msingi ni kumsikiliza kwa makini na kujitahidi kufuata nyayo zake. Kamwe Yesu hatawaacha peke yao hata katika shida na mahangaiko yao ya ndani, kwani Yesu ni nguzo ya matumaini kwa wafuasi wake.

Baba Mtakatifu anasema, katika Ibada ya Makaribisho kwa Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwenye ufuko wa Copacabana, Alhamisi, tarehe 25 Julai 2013 atapata nafasi ya kuweza kufafanua kwa kina zaidi kuhusu ukweli huu, ili kutoa mwanga angavu katika hija ya maisha ya vijana.







All the contents on this site are copyrighted ©.