Utengano ndani ya Kanisa unaweza kupatiwa tiba kwa njia ya huruma ya Mungu
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa vatican ni fursa ya kuangalia mchango wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican
katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Mababa 200
kutoka Kanisa la Mashariki walihudhuria Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakaweka msingi
wa ushirikiano na majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa.
Ni Mababa ambao
wamechangia kwa namna ya pekee, katika Maadhimisho haya wakitambua dhamana yao katika
kujenga na kudumisha uhusiano ndani ya urika wao kama Maaskofu, kielelezo cha umoja
katika Makanisa mahalia pamoja na Kanisa la Kiulimwengu wanapoungana na Khalifa wa
Mtakatifu Petro ambaye ni kielelezo cha kifungo cha amani, upendo na umoja. Maaskofu
wote wanawajibika kukuza na kulinda umoja wa imani na nidhamu pamoja na mshikamano
wa upendo kwa maskini na wote wanaodhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia.
Maaskofu
wanapaswa kushikamana kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya
dunia. Utofauti wa Makanisa mahalia yaliyo na umoja kati yao unadhihirisha zaidi Ukatoliki
wa Kanisa lisilogawanyika.
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia
umuhimu wa Kanisa kuendelea kuhamasisha umoja na udugu kwa Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga
ili kuweza kuungana kiimani kwa kuzingatia kanuni na sheria za Kanisa zilizopo. Kuna
uwezekano pia kwa Waamini wa Kanisa la Mashariki kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho
ya Mafumbo ya Kanisa.
Useja na Ndoa kwa Makleri wa Kanisa la Mashariki ni
sehemu ya wito wao unaopaswa kuheshimiwa katika mchakato wa kujenga na kuimarisha
Kanisa la Kristo. Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kunako mwaka 1990 aliridhia Sheria
za Kanisa la Mashariki, kiini cha sheria hizi ni umoja na mshikamano na Khalifa wa
Mtakatifu Petro.
Ni mchango wa Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza
la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano
kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kama ulivyoandaliwa na Ubalozi wa Romania mjini
Vatican. Juhudi za majadiliano ya kiekumene zinapania pia kuchota utajiri mkubwa unaopatikana
katika Liturujia ya Makanisa ya Mashariki; maisha ya kiroho, nidhamu na taalimungu.
Katika utofauti huu utume na ukatoliki wa Kanisa unajidhihirisha wazi; kila
upande ukiwa na haki sawa pamoja na dhamana ya kutekeleza. Huu ulikuwa ni mchango
mkubwa uliotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mambo yote haya anasema
Kardinali Sandri yanaratibiwa na mwongozo uliotolewa na Bara la Kipapa kwa ajili ya
Makanisa ya Mashariki mwa Mwaka 1996 unaozingatia pia Sheria za Kanisa la Mashariki
kwa kuhimiza uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Neno la Mungu halibadiliki, lakini
mwanadamu anabadilika kutokana na historia na nyakati, changamoto ya kusoma alama
za nyakati.
Kwa muhtasari Kardinali Sandri anasema haya ndiyo mawazo makuu
yaliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuonesha kwanza kabisa:
maisha ya kiroho yanayofumbatwa katika sala na Mapokeo ya Kanisa la Mashariki, daima
iwe n changamoto kwa waamini kutafuta Umoja wa Kanisa. Utengano ndani ya Kanisa unaweza
kupatiwa tiba kwa njia dawa ya huruma ya Mungu, kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu
Yohane wa Ishirini na tatu.
Dhambi na upotofu virekebishwe; mdhambi aonjeshwe
upendo na huruma ya Mungu. Kwa pamoja, Makanisa haya yajikite katika mchakato wa Uinjilishaji
kama alivyobainisha Papa Paulo wa Sita; changamoto inayoendelezwa na Mama Kanisa kwa
sasa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Kardinali Sandri anasema kwamba,
umoja wa Kanisa ndiyo changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi na Makanisa kwa
njia ya ushuhuda wa imani katika matendo. Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki ni amana
kubwa kwa Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Wakristo wanapaswa
kuonesha ushindi wa Msalaba wa Kristo, chemchemi ya huruma, upendo na wokovu kutoka
kwa Mwenyezi Mungu. Umoja na Mshikamano wa Wakristo uwe ni jukwaa la kukoleza pia
majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine, ili dunia iwe ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi.