2013-07-25 09:03:00

Kanisa linahamasishwa kumwilisha imani katika matendo!


Mama Kanisa anachangamotishwa na Kristo mwenyewe kuhakikisha kwamba, anamwilisha dhana ya Msamaria mwema katika maisha na utume wake kama njia ya kupambana na vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa misingi ya haki na amani, kwa kuonesha umuhimu wa Fumbo la Msalaba.

Uinjilishaji daima unakwenda sanjari na mikakati ya maendeleo endelevu inayopania kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, daima heshima na utu wa binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Huu ndio ushuhuda unaoneshwa na Hospitali ya Mtakatifu Francisko iliyofunguliwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Siku a Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Ni hospitali inayotoa huduma kwa vijana walioathirika na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Vijana watakaobahatika kupona na kurudi katika maisha ya kawaida, kwa hakika watakuwa ni matunda ya Uinjilishaji wa kina, unaoliwezesha Kanisa kuwamegea watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa kidugu na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Hizi ni jitihada za Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha ushuhuda wa imani katika matendo! Ni mwaliko wa kuendeleza ile huruma ya Mwenyezi Mungu kwa wote wanamkimbilia wakitaka kuonja tena upendo wake baada ya kuathirika kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Oran Joao Tempesta, Jumatano tarehe 24 Julai 2013 mbele ya Baba Mtakatifu Francisko katika ufunguzi wa Hospitali ya Mtakatifu Francisko, maalum kwa ajili ya wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili; vijana wanaojitahidi kujiondoa kutoka katika utumwa na mnyororo wa matumizi haramu ya dawa za kulevya. Ujenzi wa Hospitali hii ni matunda ya ushirikiano kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Kanisa Katoliki nchini Brazil.

Vijana wengi waliotoa ushuhuda wao wanasema, uchaguzi wa jina la Francisko uliofanywa na Baba Mtakatifu mara tu baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa ni kielelezo makini cha mradi wa maisha unaopaswa kufanyiwa kazi, kama alivyofanya Mtakatifu Francisko aliyejitoa bila kujibakiza kwa ajili ya maskini na wagonjwa wa ukoma kwa nyakati zake.

Ni mwaliko wa kuganga miili ya watu na kuponya roho zao kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Hata leo hii, Baba Mtakatifu anaendelea kuchangamotishwa na Kristo kwa njia ya maneno ya Mtakatifu Francisko wa Assis, Jenga Kanisa langu! Hospitali hii ni shule ya utakatifu wa maisha, inayowaonjesha watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo. Hii ndiyo hamu ya Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba, Kanisa linajitosa kimaso maso kwa ajili ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kubwa nchini Brazil ambayo kwa sasa inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi wa dawa za kulevya. Kumbe, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika Hospitali hii umekuwa ni tukio ambalo linaacha chapa ya kudumu kwa Brazil, lakini kwa vijana wanaohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kutambua madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya il kamwe wasijitumbukize wala kuwatumbukiza wengine huko!







All the contents on this site are copyrighted ©.