2013-07-25 09:16:12

Injili ya Uhai na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo!


Maadhimisho ya Siku ya Injili ya Uhai, Evangelium Vitae, ilikuwa ni fursa ya pekee kabisa kwa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kupaaza sauti kwa kishindo kikuu ili kulinda na kutetea Injili ya Uhai, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. RealAudioMP3
Waamini wanasukumwa na ujumbe wa Kristo anayewaambia kwamba, amekuja ulimwenguni ili waweze kuwa na uhai.
Umati wa watu uliofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro hapo tarehe 16 Juni 2013 ni kielelezo tosha kwamba, watu wanataka kukumbatia na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya Utamaduni wa kifo. Hili ni tukio la kihistoria lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahudumu wa sekta ya afya, ambalo linaongozwa na Askofu mkuu Zygmunt Zimowski.
Ni tukio lililowakutanisha wale wote ambao katika hija ya maisha na utume wao, wanaendelea kusimama kidete kulinda na kuteteza Injili ya Uhai, tabngu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Ni watu wanaotambua na kuthamini zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni wahudumu wa sekta ya afya wanasimama usiku na mchana kusikiliza kilio cha damu!
Ni wanasiasa ambao wanaonesha msimamo thabiti kuhusu haki msingi za binadamu zinazopata chimbuko lake katika uhai wa mwanadamu; hawa anasema Askofu mkuu Zimowsiki ni watunga sera wanaotambua na kuthamini ut una heshima ya binadamu. Maadhimisho ya Injili ya Uhai sanjari na Mwendelezo wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yanapata chimbuko lake katika maisha na utume wa Kristo. Mama Kanisa anatumwa kwenda ulimwenguni kote: kutangaza, kuadhimisha na kushuhudia ulimwenguni Injili ya Uhai.
Huu ni mwendelezo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu Injili ya Uhai yaliyotangazwa na kufundishwa kuanzia Papa Pio wa kumi na mbili hadi Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika maisha na utume wao kwenye medani mbali mbali, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai; mwanadamu na utu wake wakipewa kipaumbele cha kwanza.
Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anabainisha kwamba, Injili ya Uhai inakabiliwa na vitisho na changamoto nyingi hasa kutokana na maboresho ya huduma katika sekta ya afya na tiba ya mwanadamu. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya tiba, jambo ambalo badala ya kusaidia kuenzi Injili ya Uhai yamekuwa sasa ni tishio kwa zawadi ya maisha. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu hayana budi kuheshimu na kuenzi zawadi ya maisha. Uzalishaji watoto kwa njia ya chupa kwenye maabara ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kimaadili; sera zainazokumbatia utoaji mimba na kifo laini, kwa wengi linaanza kuwa ni jambo la kawaida; lakini haipaswi kuwa hivi! Watu wanapenda anasa na starehe kiasi cha kuhatarisha zawadi ya maisha!
Jamii nyingi zimeanza kumezwa na malimwengu, hazitaki tena kuwaona watoto na wazee wenye ulemavu! Hii ndiyo falsafa ya mwenye nguvu mpishe, lakini waswahali wanasema, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni! Kuna baadhi ya nchi kutokana na ubinafsi na kupenda mno starehe, zimejikuta zina idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa na matokeo yake ni kwamba, kuna idadi kubwa ya wazee wanaopaswa kupewa hifadhi za kijamii.
Sera za utamaduni wa kifo zinaanza kupenyeza katika jamii, pole pole, kwa kuona kwamba, mtu mwenye ulemavu han anafasi tena katika ulimwengu huu. Haya ndiyo yanayojitokeza hata katika Jamii zile ambazo zinaendekeza imani za kishirikina, matokeo yake ni mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Zote hizi anasema Askofu mkuu Zimowski ni changamoto zinazoibuliwa kwenye sekta ya afya, uchumi na katika mipango ya maendeleo.
Kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujenga na kuimarisha majadiliano ya kina kuhusu: akili, imani na huduma kwa uhai na utu, na heshima ya binadamu mintarafu dhamiri nyofu ambayo kimsingi ni sheria ya Mungu iliyoandikwa kwenye moyo wa mwanadamu.
Katika kipindi cha miaka ishirini na minane tangu Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya lilipoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, limeendelea kujitahidi kusoma alama za nyakati kwa kuchanganua changamoto hizi katika mikakati ya shughuli za Uinjilishaji wa kina, unaomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili. Baraza linaendelea kufanya majadiliano ya kina na wanasayansi pamoja na maendeleo ya sayansi ya tiba, ili kuweza kuona maana ya maisha; kuzaliwa, kukua na kukomaa kwa binadamu; magonjwa na mahangaiko yake ya ndani hadi pale mauti yanapomfika kadiri ya Mpango wa Mungu.
Hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi zaidi na zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia, kwani Maaskofu wanauelewa mpana wa hali na maisha ya watu wao! Mabaraza ya Kipapa bado yanaendelea kuhamasishwa kuunda Tume ya Afya itakayojikita zaidi na masuala ya huduma ya afya katika nchi na majimbo yao! Wajitahidi kuunda umoja na mshikamano na wahudumu wa sekta mbali mbali zinazomhudumia mwanadamu. Ushirikiano huu unapaswa kuanzia kwenye ngazia ya Jimbo na kuendelea hadi kufikia mshikamano wa kimataifa. Watu wanaojitolea huduma ni muhimu sana ikiwa kama watashirikishwa katika mchakato huu!
Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi wa sekta ya afya linasema kwamba, Katiba ya wahudumu wa sekta ya afya iko mbioni kukamilika na hivyo wananchi watapewa, ili mwanga wa Mafundisho ya Kanisa uweze kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa kutambua kwamba, Injili ya Uhai ni kiini cha ujumbe wa Yesu kutoka katika Maandiko Matakatifu, kama alivyosema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili wakati alipokuwa anachapisha Waraka wa Injili ya Uhai kunako Mwaka 1995. Ni waraka muhimu sana kwa nyakati hizi ambako kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, inayoweza kuhatarisha maisha, utu na heshima ya binadamu.
Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.