Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kubwa miongoni mwa vijana!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni tarehe 24 Julai 2013 alitembelea na kufungua
Hospitali ya Mtakatifu Francisko wa Assisi inayowahudumia wagonjwa wa akili, madhabahu
ya mahangaiko na mateso ya mwanadamu; kielelezo cha toba na wongofu wa ndani uliofanywa
na Mtakatifu Francisko wa Assisi unaoendelezwa na wafuasi wake hadi leo hii kwa kuwamegea
wagonjwa furaha na matumaini, lakini zaidi kwa njia ya huduma makini.
Wanatambua
kwamba, kila sura ya mgonjwa inamwonesha Yesu Mteswa. Baba Mtakatifu anasema, uwepo
wake mahali hapo ni kutaka kuonesha mshikamano wa upendo unaotolewa na Mama Kanisa,
ili waonje matumaini katika hija ya maisha yao ya kila siku!
Baba Mtakatifu
anawaalika watu kujifunza kukumbatia kwani kuna hali nchini Brazil na sehemu mbali
mbali za dunia zinazohitaji kupewa kipaumbele cha pekee badala ya kuendelea kukumbatia
utamaduni wa kifo, unaofumbatwa katika uchu wa mali na madaraka kwa gharama kubwa.
Tatizo la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kubwa Amerika
ya Kusini, changamoto ya kupambana fika na janga hili kwa kujikita katika ujenzi wa
misingi ya haki; kwa kuwaelimisha vijana maana na tunu msingi za maisha ya pamoja,
sanjari na kuendelea kuwasaidia walioathirika na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Huduma hii ifanywe kwa upendo wa Kristo, kwa kujifunza kuwakumbatia wenye shida na
mahangaiko, kwa kuwaonesha ukaribu, huruma na upendo.
Baba Mtakatifu anawahimiza
waamini na watu wenye mapenzi mema, kuwasaidia kwa hali na mali wale waliotumbukia
katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili waweze kuwa na ujasiri wa kusimama
tena, wakionesha nia na utashi wa kufanya hivyo. Kila mtu anawajibika katika maisha
yake, jambo la msingi ni kuwa na ujasiri wa kutenda na hapo mtu anaweza kupata msaada.
Vijana katika hali kama hii, kamwe wasijisikie pweke, kwani Kanisa na watu
wenye mapenzi mema, wanaendelea kufanya hija pamoja nao katika shida na mahangaiko
yao ya ndani; wao wanapaswa kuwa ni watu wenye matumaini na kamwe, wasiache tumaini
hili kuporwa na wajanja wachache. Kila mwamini awe ni chombo cha matumaini kwa jirani
yake.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema kuwa ni Wasamaria wema kwa jirani zao; watu wanaoguswa na shida na mahangaiko
ya watu, kiasi hata cha kujitaabisha kuwahudumia. Hospitali ya Mtakatifu Francisko
wa Assis ni kielelezo cha huduma ya Msamaria mwema, inayomjali mtu katika mahangaiko
yake, ili hatimaye, aweze kuonja upendo. Chama cha Mtakatifu Francisko na wadau mbali
mbali wanaotoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya ni kielelezo cha watu wanaojitaabisha
kuuona uso wa Kristo anayeteseka. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wote kwa moyo
wa dhati kabisa! Hii ni huduma wanayoitekeleza kwa ndugu zake Kristo.
Mwishoni,
Baba Mtakatifu anawaalika wote kusimama kidete kupinga matumizi haramu ya dawa za
kulevya; daima Kanisa litaendelea kuwasaidia katika shida na mahangaiko yao na kwamba,
Kristo awe ni faraja na tumaini la maisha yao. Bikira Maria ataendelea kuwasaidia
kubeba Msalaba kwa imani na matumaini.