2013-07-24 16:42:35

Dumisheni matumaini, mwachieni Mungu nafasi kati maisha yenu ili awashangaze mpate kuishi kwa furaha!


Katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida, takribani miaka sita iliyopita, Shirikisho la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi lilikusanyika katika Maadhimisho ya Mkutano mkuu, uliowakirimia fursa ya kupembua kwa kina maana na umuhimu wa kukutana na Kristo, ufuasi na utume ambao ulikuwa mbele yao. Mkutano ule, lilikuwa ni tukio muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini.

Matunda makubwa ya kazi iliyofanywa na Maaskofu ni matokeo ya mwingiliano kati ya viongozi wa Kanisa na mahujaji wa kawaida wanaoendelea kumiminika katika Madhabahu haya chini ya ulinzi wa Bikira Maria. Kanisa linapomtafuta Yesu, kwanza kabisa linabisha mlango kwa Bikira Maria ili aweze kuwaonesha Yesu, ili kujifunza kuwa kweli ni wafuasi waaminifu wa Yesu, ndiyo maana Kanisa katika utume wake, linaendelea kufuata nyayo za Bikira Maria.

Ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida, ili kuombea mafanikio Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, yalimwezesha kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kutembelea nchini Brazil. Anamwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia viongozi wa Kanisa, wazazi na walezi wa vijana waweze kuwa makini katika kurithisha tunu msingi za maisha kwa vijana wa kizazi kipya, daima wakitambua kwamba, wao ni wajenzi wa taifa na ulimwengu ambao unasimikwa katika msingi wa haki, mshikamano na udugu.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anawataka waamini waendelee kujikita katika mambo makuu matatu: matumaini, huku wakimwachia Mungu ili aendelee kuwashangaza pamoja na kuishi kwa furaha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kulinda na kudumisha matumaini kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya madhulumu, mateso na mahangaiko wanayokabiliana nayo, kwani kamwe Mwenyezi Mungu hataweza kuwaacha wahangamie. Waamini wasikate tamaa na watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kufanya hija pamoja nao katika kila hatua ya maisha, kamwe hawezi kuwaacha na hivyo hakuna haja ya kukata tamaa na kupoteza matumaini.

Maovu yamo katika maisha, lakini Mungu ana nguvu zaidi na ndiye chemchemi ya matumaini haya! Vijana wanakabiliwa na changamoto katika maisha, wanavutwa na hamu ya kutaka kuwa na fedha, mafanikio, nguvu, raha na starehe, lakini kwa bahati mbaya, vijana wengi wanajikuta wanakumbana na upweke hasi, unaowaonjesha ukakasi wa maisha, kiasi cha kukata tamaa na kuanza kutafuta njia mbadala.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa ni mwanga wa matumaini kwa wale waliokata tamaa, wawe ni kielelezo cha ukarimu miongoni mwa vijana na wawe tayari kuwasaidia vijana katika mchakato wa ujenzi wa dunia iliyo bora zaidi. Vijana ni nguvu na jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana waonjeshwe tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zinazofumbatwa katika: maisha ya kiroho, ukarimu, mshikamano, udumifu, udugu na furaha mambo msingi katika imani ya Kikristo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaomba waamini kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi, ili aweze kuwashangaza katika maisha, wakitambua kwamba, imani ni chimbuko la matumaini hata katika shida na mahangaiko ya mwanadamu. Historia ya Madhabahu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni kielelezo cha matendo makuu ya Mungu kwa mwanadamu.

Hapa ni mahali ambapo wananchi wa Brazil wanajisikia ni watoto wa Mama mmoja, mwaliko kwa waamini kumwachia Mwenyezi Mungu nafasi katika mioyo yao ili aweze kuwaonjesha upendo, matumaini na furaha, kiasi kwamba: ubaridi wa maisha, mateso na dhambi zinageuka kuwa ni fursa ya kujenga uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kwa namna ya pekee kutembea katika matumaini huku wakionesha ile furaha ya ndani inayobubujika kutoka kwa Yesu, kwani furaha ni sehemu ya vinasaba vya Mkristo na kamwe Mkristo hapaswi kuwa na uso uliokunjamana! Bikira Maria daima anawaombea watoto wake na kwamba, Yesu amewafunulia wafuasi wake uso wa Mungu mwenye upendo na huruma. Dhambi na mauti vimeshindwa, mwaliko kwa kila mwamini kuonesha upendo wa pekee kwa Kristo, huku wakiwaonjesha wengine furaha inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao. Kristo ni upendo, tumaini na mwanga wa waamini kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Baba Mtakatifu anawaambia waamini kwamba, baada ya kubisha hodi na kufunguliwa mlango na Bikira Maria, ni zamu yao sasa kuwa makini kusikiliza yale watakaoambiwa na Bikira Maria, ili waweze kuyatekeleza kwa matumaini kwani njia za Mungu zinasheheni furaha!







All the contents on this site are copyrighted ©.