2013-07-24 09:19:47

Amani ya kweli Mashariki ya Kati inapatikana kwa njia ya majadiliano na upatanisho wa kweli!


Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa anasema kwamba, ujumbe wa Vatican unapenda kutoa kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo ya wananchi wa Syria katika ujumla wao.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, majadiliano ya kisiasa kati ya Waisrael na Wapalestina yataanza, lakini zaidi, Baba Mtakatifu Francisko ameonesha kuguswa kwa namna ya pekee na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Syria. Damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika na watu wenye mapenzi mema wanajiuliza hadi lini vitendo hivi vitaweza kusitishwa ili watu waweze kuishi kwa amani na utulivu.

Askofu mkuu Chullikatt anasema kwamba kuna zaidi ya wakimbizi millioni 1.8, sawa na asilimia 10% ya idadi ya wananchi wote wa Syria, wanaotafuta hifadhi, amani na utulivu kwa nchi jirani. Taarifa zinaonesha kwamba, kuna jumla ya watu millioni 4 ambao hawana makazi maalum nchini Syria, hii ni sawa na asilimia 18 ya idadi ya wananchi wa Syria. Wakimbizi millioni 6.8 wanahitaji msaada wa dharura, baada ya makazi yao kuharibiwa vibaya na vita inayoendelea nchini Syria, kiasi cha kutishia amani na usalama katika Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Askofu mkuu Chullikatt anakiri kwamba, vita ina madhara makubwa kwa wote, lakini Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya Kati wanaathirika zaidi, kiasi cha kutishia amani na uwepo wao wa zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Wakristo wanadhulumiwa, wananyanyaswa na wengine kuuwawa kikatili kutokana na imani yao. Zaidi ya Makanisa 60 yameharibiwa vibaya katika siku za hivi karibuni, kiasi cha kuharibu urithi na utamaduni uliokuwa unahifadhiwa kwenye Makanisa haya, si tu kwa ajili ya Wakristo, bali kwa binadamu wote!

Ujumbe wa Vatican katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unasema kwamba, hakuna maendeleo endelevu pasi na kukazia misingi ya haki na amani miongoni mwa Jamii, kila mtu akiheshimiwa na kuthaminiwa hata katika tofauti za kiimani zinazojitokeza.

Hii ni changamoto ya kuanzisha majadiliano yanayopania kuleta upatanisho wa kitaifa miongoni mwa wananchi wa Syria. Wahusika wa machafuko na vita hii wafikishwe mbele ya mkondo wa sheria na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa idhibiti biashara ya silaha inayoendelea kuleta maafa makubwa kwa wananchi wa Syria.

Askofu mkuu Francis Chullikatt anasema, amani ya kweli huko Mashariki ya Kati inaweza kupatikana kwa njia ya majadiliano na upatanisho wa kitaifa, kwa kuonesha utashi wa kisiasa katika mchakato wa kukomesha vita hii. Wadau wakuu watambue na kuthamini umuhimu wa majadiliano kama njia ya kupata amani ya kweli, kila upande ukichunguza dhamiri yake kuhusu uvunjifu wa misingi ya haki na amani wanayoifanya dhidi ya wananchi wa Syria. Chuki na hali ya kulipiza kisasi vitaendelea kuleta maafa makubwa nchini Syria.







All the contents on this site are copyrighted ©.