Vijana angalieni kwa umakini madhara ya utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia!
Ndugu Francis Kilenga kutoka Dar es Salaam katika mahojiano na Radio Vatican anasema,
dunia ni tambara bovu na ni sawa na mti mkavu! Vijana wanapaswa kuwa makini katika
ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kamwe wasipende kujiingiza
katika mambo ambayo yanaweza kuwapeleka pabaya!
Athari za
utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia zimekuwa ni chanzo kikuu cha kumong'onyoka
kwa misingi bora ya maadili na utu wema! Vijana wengi wanapenda kufuata na kuiga mkumbo
wa yale wanayoyaona kwenye mitandao ya kijamii, matokeo yake ni kukosa dira na mwelekeo
katika maisha.
Ndugu Francis Kilenga vijana wawe makini kwa mila na desturi
njema za Kiafrika na Kitanzania, wawe na msimamo thabiti katika maisha ya kiroho na
kimaadili, kamwe wasikubali kuyumbishwa kinyume cha utashi na msimamo wao wa maisha
adili na manyofu. Vijana wamebarikiwa kuwa na karama na vipaji mbali mbali ambavyo
vinapaswa kutumiwa kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa, Familia na Jamii katika ujumla wake.
Ndugu Francis Kilenga, akizungumzia kuhusu Familia anasema, anapenda kuzihamasisha
familia kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa kama sehemu ya mchakato wa kukamilisha
utu na heshima yao kama binadamu. Ikumbukwe kwamba, kazi ni msingi wa maisha na uhai
wa mwanadamu. Kazi itekelezwe kwa nidhamu na uaminifu mkubwa na kwa njia hii waamini
wanaweza kutolea ushuhuda amini na mwenye mashiko kwa wale wanaowazunguka.
Hii
ndiyo changamoto ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na kwa namna ya pekee, wakati huu
vijana wanapoadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa huko Rio de Janeiro, Brazil.