2013-07-23 11:32:51

Rais Kikwete akutana na Bwana Andry Rajoelina


Rais wa Serikali ya Mpito ya Madagascar, Andry Rajoelina amewasili nchini kwa ziara ya kikazi nchini Tanzania ambako baadaye atakuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar Es Salaam, Rajoelina amepokelewa na mwenyeji wake, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC-Troika) ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Rais Kikwete ndiye amepewa jukumu na viongozi wenzake wa nchi wanachama wa SADC kutafuta suluhisho la mgogoro wa kisiasa katika Kisiwa cha Madagascar.

Viongozi hao wawili wamekutana Ikulu, Dar es Salaam ili kuzungumzia hali ya kisiasa nchini Madagascar ambako Rais Kikwete atamweleza Rajoelina kuhusu matokeo ya kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Asasi (SADC-Troika-Summit) kilichofanyika chini ya uenyekiti wake juzi, Jumamosi usiku, mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Naye Raojelina anatarajiwa kumwelezea Rais Kikwete kuhusu hali ilivyo katika Madagascar na hasa kuhusiana na jitihada za kuandaa Uchaguzi Mkuu nchini ambao umekuwa unakumbwa na changamoto kadhaa.








All the contents on this site are copyrighted ©.