Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 22 Julai 2013 amewasili nchini Brazil na
kupokelewa na viongozi wa Serikali, Kanisa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamejipanga
kwenye barabara mbali mbali za mji wa Rio de Janeiro, kiasi kwamba, wakati mwingine
msafara wa Baba Mtakatifu ulilazimika kusimama ili kusalimia wananchi waliokuwa na
shauku na kumwona Baba Mtakatifu Francisko.
Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kumwezesha kufanya hija ya kwanza ya kitume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro
nchini Brazil ambayo imekuwa na uhusiano wa pekee na viongozi wa Kanisa hasa kutokana
na imani na urafiki wao na kwamba, yuko mbele yao akigonga mlango wa mioyo yao, akitaka
afunguliwe ili aweze kuishi pamoja nao katika kipindi hiki cha juma zima, kama sehemu
ya Maadhimisho ya Juma la Vijana Duniani.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake
anasema, hana fedha wala dhahabu, bali ndani mwake ana mbeba Yesu Kristo na yuko kati
yao kwa jina lake, ili aweze kuwashirikisha mwali wa upendo wa kidugu unaowaka katika
mioyo ya wengi na kwamba, anamtakia kila mmoja wao amani ya Kristo! Baba Mtakatifu
anawashukuru viongozi wa Serikali na wadau mbali mbali waliowezesha hija yake ya kichungaji
nchini Brazil.
Amewasalimu na kuwapongeza Makleri nchini Brazil kwa huduma
makini wanayotoa kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini humo. Anasema, uwepo wake miongoni
mwao unalenga kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo yanayobubujika
kutoka kwa Kristo mwenyewe.
Baba Mtakatifu anasema hija yake ya kichungaji
inapania kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani, inayompania fursa ya pekee kukutana na
kuzungumza na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaovutwa na Kristo Mkombozi.
Hawa ni vijana wanaotafuta hifadhi katika Moyo wake Mtakatifu pamoja na kusikiliza
ule wito wake unaowachangamotisha kwa kusema "Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote
kuwa wanafunzi".
Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanazungumza lugha
mbali mbali na kutoka katika tamaduni tofauti, lakini kwa pamoja wanashikamanishwa
na matumaini yao kwa Kristo anayeweza kuzima kiu ya ukweli na upendo licha ya tofauti
zinazojitokeza kati yao.
Yesu anatoa nafasi ya kuweza kujenga na kudumisha
urafiki na vijana hawa, ili hatimaye, waweze kuwa ni wadau wakuu wa uinjilishaji unaopania
kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu. Vijana wako tayari kujitosa
kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwani wanatambua kwamba, kamwe hataweza
kuwaangusha!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, anapozungumza na vijana anatambua
kwamba, anazungumza pia na wazazi, jumuiya na makanisa yao mahalia. Vijana ni tumaini
la Jamii kwa sasa na kesho iliyo bora zaidi, changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanathaminiwa
na kutunzwa vyema, kama ilivyo mboni ya jicho! Vijana ni kama dirisha linaloruhusu
mambo ya ulimwengu ujao kuweza kupenya, hali inayoibua changamoto nyingi.
Vijana
wanahitaji nafasi, hivyo ni jukumu la Jamii kutoa fursa hizi: kiroho na kimwili, ili
waweze kujenga msingi wa maisha yao; wakiwa na usalama na uhakika wa maisha kwa njia
ya elimu makini; kwa kuwarithisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Kwa hakika
vijana wanapaswa kupewa maisha bora, kwa kuamsha karama na vipaji walivyonavyo ili
kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa hatima yao ya maisha, wakiwajibika pia kwa
ajili ya mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kuwataka
wahusika mbali mbali kuwa karibu na vijana ili kujenga urafiki utakaosaidia kuanzisha
majadiliano na vijana. Upendo wake unawakumbatia na kuwafunika wananchi wote wa Brazil
katika tamaduni na utajiri walio nao. Anasema, atapata nafasi ya pekee kwa ajili ya
kusali na kuwaombea kwa Bikira Maria wa Aparecida, akiwaombea ulinzi na tunza ya kimama
kwa ajili ya nyumba na familia zao. Baba Mtakatifu anawashukuru wananchi wa Brazil
kwa mapokezi makubwa waliyomkirimia!