Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na changamoto zake nchini Tanzania
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, utekelezaji
wake unafanyika katika ngazi ya Majimbo na hapo Novemba, Maaskofu wote watakusanyika
Mji mkongwe wa Bagamoyo kwa muda wa siku tatu, ili kuadhimisha Mwaka wa Imani. Bagamoyo ni mahali
ambapo Imani ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania ilipata chimbuko lake. Hii itakuwa
ni fursa kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania kufanya tafakari ya kina kuhusu Kanuni
ya Imani kwa kuyahusisha makundi mbali mbali ndani ya Kanisa kadiri ya mahitaji na
usomaji wa alama za nyakati. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Familia ya Mungu nchini
Tanzania, ni toba na wongofu wa ndani kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza,
kwa njia ya ushuhuda na utakatifu wa maisha. Waamini wanaendelea kuchangamotishwa
kujikita katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, kama njia ya
kumsogelea Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao! Askofu Ngalalekumtwa anasema
wakati huu wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani, ujumbe kwa vijana ni kutubu
na kumwongokea Mungu, kwani ujana kwa sasa umekuwa nongwa! Wanapaswa kujichunga ili
kamwe wasiharibu ujana wao kwa maisha yasiyo adili. Vijana wanaendelea kukabiliana
na changamoto za maisha: kiuchumi, kiimani, kimaadili na kiutu. Wengi wao hawana fursa
za ajira na matokeo yake ni kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria,
utu na maadili mema. Vijana wanapaswa kulelewa kiroho, wajengewe ujasiriamali na wapewe
nafasi ya kujifunza ufundi ili waweze kujiajiri wenyewe. Tanzania baada ya kukaa
kwa amani na utulivu kwa takribani miaka 50, kwa siku za hivi karibuni imejikuta ikikabiliana
na changamoto za uvunjifu wa misingi ya haki na amani ambayo imesababishwa na lugha
za uchochezi, madhulumu na mashambulizi ya kidini, kiasi kwamba kuna baadhi ya viongozi
na waamini wamepoteza maisha yao. Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha
haki msingi za binadamu. Uchochezi unaofanywa na watu wa nje kwa malengo yao binafsi
udhibitiwe na kamwe vijana wasikubali kutumiwa na watu wenye nia mbaya kutokana na
umaskini wao ili kuvuruga misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa
kwa kupokea “vijisenti” ili wafanye vurugu. Askofu Ngalalekumtwa anawataka watu
hao wanaotumia vibaya utajiri na mali yao, kuwajengea uwezo vijana badala ya kusababisha
maafa na uvunjifu wa misingi ya haki, amani na utulivu.