2013-07-23 08:55:40

Kuna hatari ya kuwa na kizazi kisichokuwa na fursa za ajira kwa siku za usoni!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa safari yake kuelekea Brazil, alipata nafasi ya kusalimiana na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa utani amesema kwamba, yeye anajiona kama Kondoo kati ya Mbwa mwitu, lakini anadhani kwamba, si wabaya kiasi hiki. Anawaalika waandishi wa habari kumsaidia katika kutekeleza utume na wajibu wake miongoni mwa vijana.

Baba Mtakatifu anatamani kuwaona vijana wakiwa wanashirikishwa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, bila kuwatenga kwani kwa kufanya hivyo ni kutowatendea haki, hali ambayo inaweza kuwafanya vijana kukosa utambulisho unaopata chimbuko lake katika: familia, tamaduni, taifa na imani. Vijana ni matumaini na jeuri ya taifa, kwani ndani mwao wanabeba nguvu inayowasukuma kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, vijana na wazee wanapaswa kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jamii husika. Wazee wanaoutajiri mkubwa na amana wanazobeba katika maisha yao; wao ni chemchemi ya maisha, hekima, historia na tunu msingi za maisha ya kifamilia. Hii ndiyo hazina ambayo wazee wanapaswa kuwarithisha vijana.

Idadi ya vijana wasiokuwa na fursa za ajira anasema Baba Mtakatifu ni kubwa mno kiasi kwamba, kuna hatari ya kuwa na vijana wa kizazi kipya wasiokuwa na fursa za ajira. Kazi ni jina na utambulisho wa mtu; kazi ni utimilifu wa maisha na utu wa binadamu; kwa njia ya kazi, mwanadamu anaweza kujipatia mahitaji yake msingi. Kwa sasa vijana wengi wamechanganyikiwa kwa kukosa fursa za ajira. Watu wengi katika ulimwengu wa utandawazi wamezoea utamaduni wa kuwatenga watu, jambo ambalo limepitwa na wakati. Kuna haja ya kujenga utamaduni wa majadiliano na kushirikishana watu wengi zaidi katika maisha ya kijamii.

Baba Mtakatifu anasema, hamu yake kuu ni kutaka kuona kwamba, vijana wanashirikishwa katika maisha ya kijamii bila kutengwa, huu ndio ujumbe ambao anapenda kuwapatia vijana na jamii kwa ujumla katika Maadhimisho ya Juma la Vijana kwa Mwaka 2013 linalofanyika nchini Brazil. Baada ya mazungumzo haya kwa waandishi wa habari, Baba Mtakatifu alipata fursa ya kuweza kuzungumza na kila mmoja wao na hivyo kuweza kubadilishana mawazo.

Msafara wa Baba Mtakatifu ulikuwa na jumla ya waandishi habari 70 kutoka katika vyombo mbali mbali vya habari, kitaifa na kimataifa. Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kwa niaba ya waandishi wa habari walioko kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru kwa fursa hii na kwamba, waandishi wa habari watakuwa ni wenza waaminifu katika hija yake ya kitume nchini Brazil. Baba Mtakatifu anawaomba wafanye hivyo kwa ajili ya mafao ya wengi!







All the contents on this site are copyrighted ©.