2013-07-23 10:11:33

Athari za biashara haramu ya dawa za kulevya duniani!


Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa hivi karibuni alishiriki kikamilifu kwenye mkutano wan ne wa Bara la Amerika ya Kusini na Kaskazini, uliofanyika mjini Antiqua, Guatemala, ili kujadili mwelekeo wa sera makini Barani Marekani dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya. RealAudioMP3
Hii inatokana na ukweli kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa watumiaji, familia na jamii katika ujumla wake. Biashara haramu ya dawa za kulevya ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa inayopania pamoja na mambo mengine kuwasaidia waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa lengo la kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Kuna idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha na matumaini kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu unatambua umuhimu wa Familia kama msingi wa mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kuleya, kwani madhara yake ni makubwa kwa Jamii, changamoto kwa watunga sera kutoa kipaumbele cha pekee katika kuenzi tunu msingi za maisha ya kifamilia.
Hapa ni mahali ambapo waathirika wanaweza kupata mbinu za kujikinga na matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwa wale ambao wamekwisha athirika, Familia inakuwa ni mahali pa kwanza kabisa pa kuweza kupata tiba na kuonja tena upendo wa kifamilia unamrudishia mwathirika ile dhamana na nafasi yake ndani ya Jamii.
Familia haina budi kutazamwa katika mapana yake, anasema Askofu mkuu Chullikatt. Uchunguzi wa athari za matumizi haramu ya dawa za kulevya unaonesha kwamba, watoto wanaozaliwa na kuishi katika mazingira bora ya kifamilia wanao uwezo mkubwa wa kupambana na kishawishi cha matumizi haramu ya dawa za kulevya, ikilinganishwa na watoto wanaozaliwa katika familia tenge. Waathirika wanahitaji kwa namna ya pekee kuonja upendo kutoka katika familia zao. Utu na heshima ya vijana inapaswa kulindwa na kuheshimiwa kwani hawa ni rasilimali watu na tegemeo la Jamii kwa siku za usoni.
Vijana wafundishwe kuhusu madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwamba, wajengewe uwezo wa kupambana fikan a athari za matumizi haramu ya dawa za kulevya, sanjari na kupewa tiba wale ambao tayari wametumbukizwa au kujitumbukiza katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kupewa tiba, kutunzwa na kuungwa mkono katika mchakato wa kuondokana na utumwa huu miongoni mwa vijana wa kizazi kipya!
Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu umekazia umuhimu wa kuwaundia vijana dhamiri nyofu yenye uwezo wa kutambua mema ya kufuata na mabaya yanayopaswa kuepukwa! Kuna haja ya kuwa na jukwaa linaloweza kujadili kwa kina na mapana kuhusu madhara ya biashara haramu ya dawa za kulevya na makosa ya jinai pamoja na kuangalia uwezekano wa kuweka mikakati itakayosaidia kudhibiti ongezeko la ugavi wa dawa haramu za kulevya kwenye soko la kimataifa.
Jamii inapaswa kujikita zaidi na zaidi katika misingi ya haki, amani nau salama. Wajijengee utamaduni wa kujiamini kwa kutambua kwamba, matumizi haramu ya dawa za kulevya ni chimbuko la mateso na mahangaiko yao ya ndani. Mikakati na sera za mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya hazina budi kuzingatia maisha ya mwanadamu ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, mwanadamu: roho na mwili anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Vijana ni rasilimali watu inayohitajika kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa sasa na kesho iliyo bora zaidi
Askofu mkuu Francis Chullikatt anasema kwamba, ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kimaadili kupambana na biashara haramu ya dawaza kulevya kwa kuangamiza uhai wa binadamu. Utu na heshima ya binadamu ni tunu zinazopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kudumishwa. Biashara haramu ya dawa za kulevya mara nyingi inakwenda sanjari na utamaduni wa kifo, unaohamasisha watu kupenda mno anasa na hatimaye, kuitema zawadi ya maisha kwa vitendo vya utoaji mimba.
Ujumbe wa Vatican unaungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Guatemala kupinga mambo yanayohusu ngono kutokana na kukinzana na sheria za kimataifa, maadili, utu wema na tunu msingi za maisha ya kijamii, kitamaduni na kiroho. Haki msingi za binadamu zinafumbata: maadili, utu na heshima ya binadamu mwenyewe, kinyume cha hapa ni ubatili mtupu!
Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha watu kuendelea kujenga utamaduni wa majadiliano ambayo ni daraja linalowaunganisha watu wenye mawazo na maoni tofauti, kiasi kwamba, watu wanaonana kana kwamba, ni ndugu wamoja, wanaopaswa kukaribishwa na kukumbatiwa na kamwe wasionekane kuwa ni maadui.
Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kuimarisha udugu na mshikamano kati ya watu na mataifa, ili kupambana kufa na kupona na changamoto zinazojitokeza kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Askofu mkuu Francis Chullikatt, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, binadamu ni rasilimali kubwa inayopaswa pia kuheshimiwa na kuthaminiwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.