Wamissionari wanatumwa kwenda kujifunza mahangaiko ya watu!
Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., limehitimisha mkutano wake
mkuu kwa kujiwekea malengo wanayopaswa kuyatekeleza katika kipindi cha miaka sita
yaani: 2013 hadi mwaka 2019. Ndani ya viunga vya Radio Vatican, tunaye Padre Felix
Mushobozi, Katibu mkuu aliyemaliza muda wake anayejuza zaidi yale yaliyojiri katika
mkutano mkuu wa ishirini, uliokuwa unafanyika mjini Roma. Jumuiya ya Wamisionari
wa Damu Azizi ya Yesu ni Ushirika wa Mashahidi wa Kristu wenye kutoka katika tamaduni
tofauti ulimwenguni; kwa lengo la kuhamasisha majiundo mapya katika Kanisa na kwenye
mazingira tunamoishi. Kutokana na mwongozo huu, wajumbe wa mkutano mkuu wa 20 waliokutana
mjini Roma kuanzia tarehe 8 hadi 19 mwezi Julai, 2013 wamemchagua Padre William Nordenbrock
kutoka Kanda ya Cincinnati (Marekani), kuwa mkuu mpya wa shirika, baada ya Pd. Francesco
Bartoloni kumaliza muda wake wa uongozi. Kabla ya uchaguzi, mkutano mkuu uliweka
bayana Dira itakayoongoza shirika kwa kipindi cha miaka sita ijayo, yaani kuandia
2013 hadi 2019. Umoja: tunasisitiza maisha ya pamoja ili kama Wamisionari
tuweze kuishi vema karama za kiutu na kiroho tulizotunukiwa na Mwenyezi Mungu. Tunajitahidi
kuishi karama za shirika kwa ajili ya uenjilishaji na utume ndani ya Kanisa na ulimwengu. Utume
na Uinjilishaji: Upendo wa Kristo unaojidhihirika katika fumbo la Msalaba kwa kumwaga
damu yake Azizi, ndio unaotubidiisha katika uenjilishaji na utume wetu popote tunapotumwa. Utume
wa Neno la Mungu: Hii ndiyo karama kuu ya shirika letu zinamojikita karama nyingine
zote. Kwa maana hii ni kwamba sisi Utambulisho wetu ni Umissionari tukiwa na maana
sisi ni wahubiri wa Neno la Mungu – Kwa maneno na kwa ushuhuda wetu tukijaribu kusikiliza
na kujibu Vilio mbalimbali vya Damu ya Kristo: Katika Uenjilishaji tunajitambua
kuwa tumeitwa kupeleka Upatanisho ambao Kristo alikuja kuuleta mahali popote ambapo
kuna mipasuko ya kila aina: kiroho, kimwili, kimaadili, kijamii, kisiasa, kiuchumi,
katika mazingira na viumbe ambavyo Mwenyezi Mungu ametukabidhi vitumike kadiri ya
mpango wake. Upatanisho: Lengo letu ni kuhakikisha kuwa katika ulimwengu na kanisa
Upendo na huruma ya Mungu vinawaletea watu Uponyaji na ukombozi. Magonjwa ya kila
aina yaweze kupata tiba toka kwa Damu ya Yesu; Watu wa kila jamaa, lugha, kabila na
taifa wanakombolewa kutoka utumwa wa shetani na ubabe wa kila aina. Tunatumwa hasa
kwenda hadi pembezoni mwa Jamii na Kanisa: Katika maana aliyoeleza Baba Mt. Francisko
toka alipoanza utume wake kama Askofu wa Roma na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba
Mtakatifu alituhimiza kutoka katika sakristia zetu na kwenda huko ambako watu wenye
vilio mbalimbali waliko. Kwenda mpaka pembezoni mwa mwa jamii. Alihimiza kuwa
na mtazamo wa kanisa kwa ajili ya maskini na walalahoi. Huu ndio wito na utume wa
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Katika mkutano wetu tumeona kuwa kazi ya Umisionari
itakuwa na ufanisi kama tutaifanya kwa ushirikiano wa karibu na walei – watu wa kawaida
wanaomwamini Kristo na kushiriki utume wake kama Wabatizwa. Wao wako kwenye nafasi
nzuri ya kuelewa uchungu wa maisha ya kawaida kuliko sisi makleri ambao mara nyingi
tunahubiri toka juu ya mimbari bila kushuka chini na kuhisi matatizo ya watu wa kawaida.
Tunahimizwa basi kwenda kushiriki mahangaiko ya watu pale wanakoishi. Tunaitikia
mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko aliposema mchungaji hana budi kwenda kushiriki
harufu ya kondoo wa Bwana.