Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Jopo la waandaaji wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani kwa Mwaka 2013, wanaendesha majadiliano ya kina miongoni mwa vijana kuhusu
dhamana na wajibu wao katika medani ya uongozi katika mchakato wa maendeleo endelevu
na amani.
Tarehe 23 Julai 2013, kunafanyika tamasha linaloongozwa na kauli
mbiu “Vijana na Utamaduni wa Amani”. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika tamasha
hili anawakilishwa na Bwana Ahmad Alhendawi. Katika majadiliano haya, kila Bara litakuwa
na mwakilishi mmoja mmoja.
Juma la vijana kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko
wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 21 Julai 2013 kwenye Uwanja wa
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni fursa makini ya kuwasikiliza na kuzungumza
na vijana kutoka pande mbali mbali za dunia sanjari na kujifunza matarajio yao kwa
sas ana kesho iliyobora zaidi.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni jukwaa
linalotumiwa na Mama Kanisa kutoa fursa kwa vijana wanaotaka kukutana na Mwenyezi
Mungu katika hija ya maisha yao ya kiroho. Ni vijana wanaopenda kukutana na walimwengu,
lakini pia ni nafasi ya kuangalia undani wa maisha yao, tayari kujiwekea mikakati
na malengo kwa ajili ya siku za usoni.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani
tangu yaliyopoasisiwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili miaka 28 iliyopita, yamekuwa
ni chemchemi ya miito mitakatifu. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa
ni kuhakikisha kwamba, inawajibika kujenga, kuimarisha na kuboresha dunia ili iweze
kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.