"Naomba mnisindikize kwa sala, imani, toba na wongofu wa ndani wakati wa Maadhimisho
ya Juma la Vijana Duniani kwa Mwaka 2013"
Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 22 Julai 2013 asubuhi, ameanza hija yake
ya kwanza ya kimataifa nchini Brazil, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya
Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, inayoongozwa na kauli mbiu "Basi enendeni, mkawafanye
mataifa yote kuwa ni wanafunzi. Baba Mtakatifu na ujumbe wake, anatarajiwa kuwasili
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Antonio Carlos Jobim alasiri kwa masaa ya Brazil,
sawa na saa 4:00 kwa saa za Afrika Mashariki.
Akiwa kwenye Uwanja wa ndege
mjini Roma, Baba Mtakatifu amesindikizwa na Waziri mkuu wa Italia Bwana Enrico Letta,
viongozi wa Kanisa na Serikali ya Italia.
Mara baada ya Sala ya Malaika wa
Bwana, Jumapili, Baba Mtakatifu aliwashukuru waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa
wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwaomba
wamsindikize kwa njia ya sala, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Juma la Vijana
Kimataifa. Vijana ndio wadau wakuu katika Maadhimisho haya, wana shauku kubwa ya kusikiliza
Yesu anawaambia nini katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Baba Mtakatifu
anawaalika vijana wengine wote ambao hawakupata bahati ya kwenda Brazil, kuendelea
kutafakari ujumbe wa Yesu katika maisha yao, tayari kujitosa kimaso maso kwa ajili
ya huduma kwa Mungu na jirani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu aliiweka safari
na maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani chini ya usimamizi na maombezi ya Bikira
Maria anayeheshimiwa sana nchini Brazil.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi
iliyopita majira ya jioni, alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu
lililoko mjini Roma na huko alipokelewa na viongozi wakuu wa Kanisa hili. Akaenda
moja kwa moja kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, akiwa amezungukwa
na Mapadre wa Shirika la Wadominikani wanaohudumia Kanisa hapo.
Amesali katika
hali ya ukimya kwa takribani nusu saa, akaweka shada la maua na kuwasha mshumaa uliokuwepo
mahali hapo. Tukio hili limeshuhudiwa na waamini pamoja na mahujaji waliokuwepo Kanisa
hapo kwani Baba Mtakatifu Francisko alikwenda Kanisani hapo bila ya maandalizi maalum.
Amewaalika waamini waliobahatika kumsikiliza mara baada ya kuhitimisha sala zake kumsindikiza
kwa njia ya sala, imani lakini zaidi kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Baadaye,
Baba Mtakatifu alirejea tena mjini Vatican, kuendelea na maandalizi ya Jumapili na
hatimaye, hija ya kichungaji nchini Brazil.