2013-07-22 08:09:26

Matunda ya Siku ya Vijana Duniani


Sr. Anneritha Buretta, C.PS, wa Shirika la Masista wa Damu Takatifu ya Yesu, kutoka Jimbo Katoliki Moshi anayefanya utume wake nchini Msumbiji kama Mratibu wa Shule za Watoto Yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi nchini Msumbiji anasema, wito wake ni matunda ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika mjini Manila, Ufilippini kunako mwaka 1995. RealAudioMP3

Alipata nafasi ya kuzungumza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, huo ukawa ni mwanzo wa chimbuko la wito wake wa kitawa na kimissionari.

Sr. Anneritha Buretta katika mahojiano na Dr. Maria Dulce wa Idhaa ya Kireno ya Radio Vatican anasema kwamba, mradi wa watoto yatima ni mkubwa na unawahusisha watoto wengi, hivyo kuna changamoto zake katika kuhakikisha kwamba, mambo yote yanakwenda kama yalivyopangwa.

Anasema, kwa mara ya kwanza alipoambia kwamba, anahamishiwa nchini Msumbiji kama kituo chake kipya cha kazi, alipata wasi wasi kuhusu huko alikokuwa anakwenda kwani Lugha ya Kireno kwake ilikuwa ni “Mama mkwe”, lakini leo hii ni maji kwa glasi anasema ni sawa na “uji kwa kibogoyo”. Wakati anajifunza lugha, ulikuwa ni wakati mgumu kwake, lakini, ilikuwa ni fursa ya kusali na kufanya tafakari ya kina, kwani alitambua kwamba, ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliyekuwa anafahamu lugha aliyokuwa anazungumza. Alikuwa na wasi wasi kuhusu: tamaduni, mila na desturi za wananchi wa Msumbiji, lakini yote haya yalikuwa ni matatizo ya mpito!

Sr. Anneritha Buretta anasema kunako mwaka 1995 alikuwa ni kati ya wasichana wawili kutoka Jimbo Katoliki la Mbeya walioshiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Manila, Ufilippini. Alipokuwa anazungumza na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, alimwambia, nenda ukawe mmissionari kati ya watu wako, maneno ambayo yalibakiza chapa ya kudumu katika moyo na fikara zake.

Alipokuwa mjini Manila, aliguswa na maisha ya Mtawa mmoja aliyekuwa Mzee, lakini alionekana kufurahia maisha ya kitawa, akajisemea moyoni mwake, bila shaka maisha haya yana utamu wake, hadi Mtawa huyu kufikia hapa alipo hata mimi ninaweza kujitosa!

Baada ya kuweka nadhiri zake za daima kama Mtawa alibahatika kufanya utume wake nchini Tanzania na Kenya. Kunako mwaka 2012 akatumwa na Shirika lake kwenda Msumbiji. Wakati huu wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013, anapenda kuwaambia vijana kusikiliza kwa makini na kujifunza mengi kwani yote watakayosikia na kuona yataendelea kuwa ni hazina ya maisha yao kwa sasa na kwa siku za baadaye.

Kama vijana wajiwekee mikakati, malengo na vipaumbele vya maisha! Kama ni kazi, wajipangie ni kazi gani wangependa kufanya na kuanza kuchakarika kwani biashara asubuhi! Kama ni mchumba, aangalie sifa na vigezo! Majiundo makini yawasaidie vijana kujiandaa vyema kwa ajili ya maisha kwa sasa na kwa siku za usoni!








All the contents on this site are copyrighted ©.