Mheshimiwa Padre Raymond Saba, katibu mkuu mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
wakati wa hija ya maisha ya kiroho mjini Roma, Lourdes na Nchi Takatifu amesema, Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, kiwe ni kipindi cha kugundua upya, uzuri na nguvu ya imani.
Ni muda muafaka
wa kujifunza kwa makini ili kuifahamu vyema imani kwa Kristo aliyezaliwa, akateswa,
akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hili ndilo wazo msingi linalopaswa kuyaongoza
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita, sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha
kwa mara ya kwanza Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.
Padre Raymond Saba anawaalika
waamini kwa mara nyingine tena kumwomba Kristo aweze kuwaongezea imani na kwamba,
hii inapaswa kuwa ni sala ya kila siku ya mwamini. Waamini wakikosa kumlilia Kristo
ili awaongezee paji la imani, watajikuta kwamba, wanakuwa ni Wakristo wa majina, Wakristo
ambao wanaridhika kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu kila Jumapili, lakini wanashindwa
kumwilisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika matendo na uhalisia wa maisha
ya kila siku!