Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho
ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana
Msalaba, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo na huruma
ya Kristo kwa ulimwengu.
Ni ushuhuda unaoonesha kwamba, kwa njia ya mateso,
kifo na ufufuko wake, mwanadamu ameweza kukirimiwa ukombozi. Tangu wakati huo, Msalaba
huu ukajulikana kuwa ni Msalaba wa Vijana, ambao umezunguka na kuzungushwa na vijana
kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa takribani miaka 28 iliyopita.
Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, mara tu baada ya Maadhimisho ya Siku
ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2011 iliyofanyika Jimbo kuu la Madrid, Hispania, aliwakabishi
vijana wa Brazil Msalaba, uliozunguka nchini Brazil, kama sehemu ya mchakato wa Maandalizi
ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.
Itakumbukwa kwamba, Msalaba wa Vijana
tangu Mwaka 1984 Msalaba huo unahifadhiwa kwenye Kituo cha Vijana Kimataifa cha San
Lorenzo, kilichoko mjini Vatican. Msalaba huu umetembezwa sehemu mbali mbali za dunia
sanjari na Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, iliyounganishwa kwenye hija ya
Msalaba wa Vijana kwa mara ya kwanza kunako Mwaka 2003.
Msalaba wa Vijana
umekuwa ni kielelezo cha sala, dhamana ya Uinjilishaji na majadiliano ya kina kuhusu
Imani ya Kanisa Katoliki miongoni mwa vijana na watu wenye mapenzi mema. Msalaba umekuwa
ni amana ya imani na ushuhuda wa vijana kwa Kristo na Kanisa lake; ni kielelezo cha
imani, matumaini na mapendo kwa wale waliokata tamaa.
Katika Maadhimisho ya
Jubilee ya Miaka 25 ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika kunako mwaka 2009, Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwakabidhi vijana Msalaba, ili waweze
kuutembeza sehemu mbali mbali za dunia, ili vijana wa kizazi kipya waweze kugundua
tena huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, ili hatimaye,
kufufua ndani ya mioyo yao matumaini kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka
katika wafu!