Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 16 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Mpendwa mwana wa Mungu, karibuni katika tafakari Neno la Mungu, masomo ya Dominika
ya 16 ya mwaka C. Mama Kanisa leo ataka tutambue kipi kilicho cha msingi katika maisha
maisha yetu kwa ujumla na hasa maisha ya ufuasi wa Bwana. Mwinjili Luka anaweka mbele
yetu tukio la Bwana aliyetembelea kijiji cha Martha na Mariamu.
Jambo linatuongoza
kutafakari Injili, ni zile hekaheka za kila Martha na Mariamu kila mmoja wao akijaribu
kumkarimu Bwana anayeenda kuwatembelea. Katika heka heka zao kutajitokeza tofauti
na hivi kila mmoja atahangaika kadiri ya vionjo au tunaweza kusema kipaji chake. Hapa
ndipo kutakuwa chanzo cha fundisho atakalolitoa Bwana hapo baadaye.
Mpendwa
msikilizaji, dada hawa wawili wamepata malezi katika familia moja lakini kila mmoja
atajitokeza tofauti na mwingine haya ndiyo maajabu ya uumbaji. Ndiyo kusema katika
tofauti zao tunapata kuonja uasilia wa mtu mmojammoja katika kuitikia wito wa Mungu
hata kama mtu yuko katika jumuiya. Utofauti wao wawakilisha utajiri wa mwanadamu.
Mpendwa
mwana wa Mungu, tunamwona Martha ambaye kwa tabia yake anaonesha umuhimu wa kutenda
kimasomaso, yaani maisha ya kuhudumia wengine, wakati Mariamu anatangaza upande mwingine
yaani maisha ya sala na tafakari ya ndani. Mariamu anatufundisha kusikiliza na hivi
kwa njia hiyo anataka kuonesha upeo mwingine wa maisha ya mwanadamu yaani mawasiliano
na Mungu. Kwa kuwatazama hawa ndugu tayari tunazo namna mbili katika maisha yetu kadiri
ya Injili yaani KUTENDA na KUTAFAKARI. Namna hizi mbili zaweza kujenga swali: Je namna
moja ni ya maana kuliko nyingine? Kwa hakika fundisho la Bwana latuambia kuwa mifumo
hii miwili haipingani bali yakamilishana katika kufikia ukamilifu wa maisha yetu.
Mpendwa
msikilizaji, bado twajiuliza mifumo hii yategemezana kwa namna gani? Hebu tuone, katika
hali ya kawaida bila Martha Bwana asingetamani kwenda kuwatembelea hawa ndugu, maana
kuwatembelea watu maana yake kuchota furaha na kupeleka furaha. Kwa nini mtu aende
ambapo anajua hakuna huduma ya chakula, maongezi nk.
Kumbe basi, ukarimu ni
muhimu sana. Jambo jingine linalotokana na huduma ya Martha ni kwamba Mariamu asingepata
nafasi ya kumsikiliza Bwana kama Martha asingejitoa katika kuandaa meza. Kama angekuwa
peke yake angewajibika kupika na kuandaa kwa ajili ya Bwana. Ndiyo kusema, huduma
ya Martha inapata kusimikwa katika maneno ya Bwana akisema: Kama mimi niliye Bwana
nimewaosha miguu basi nanyi mkanawishane ninyi kwa ninyi, na yule mkubwa kati yenu
awe kama mdogo na anayetawala awe kama yule anayetumikia.
Mariamu anayesikiliza
Neno la Mungu anasadikika kuchagua lililo bora zaidi ni kweli lakini kama tulivyoona
linasimikwa katika msingi wa huduma ya Martha. Basi Bwana anataka kutufundisha kuwa
na uwezo wa kuona kipi ni cha msingi na kwa namna gani kukifanyia kazi na zaidi sana
wapi kinalenga katika safari nzima ya wokovu wa mwanadamu.
Kumbe, thamani ya
huduma inasimika maisha yetu lakini pia huduma bila tafakari, shughuli zetu zote zitakuwa
zimejaa utupu ambao si rahisi kuuziba na tokeo la utupu ni anguko la imani na jumuiya
ya watu kwa ujumla. Mpendwa msikilizaji, katika maisha yetu lazima tutenge muda wa
kuongea na Mungu tukiwa peke yetu au katika familia, ni lazima kuwa Mariamu mwingine!.
Hii ndiyo maana ya Jumapili, ndiyo maana ya kupokea sakramenti, ndiyo maana ya sala
za kila siku, ndiyo maana ya hija na yote yaambatanayo na maisha ya missioni. Tumsifu
Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya Cpps