2013-07-19 09:46:12

Maisha na utume wa Kanisa Katoliki Brazil


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limekwishajipanga tayari kwa ajili ya kumpokea Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani, ambayo kwa Mwaka huu inafanyika mjini Rio de Janeiro. RealAudioMP3

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atakuwa nchini Brazil kuanzia tarehe 22 Julai hadi tarehe 29 Julai, 2013, atakapokunja kirago cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani na hivyo kutoa nafasi kwa Maandalizi ya Siku kama hii sehemu nyingine duniani.

Takwimu zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil zinaonesha kwamba, Brazili ina idadi ya watu wapatao million 195, 041, 000; kati yao watu million 164,780, 000, sawa na asilimia 84.48% ni waamini wa Kanisa Katoliki. Brazil ina majimbo 274, yenye Parokia 10,802 na ina vituo vya shughuli za kichungaji 37,827. Hadi taarifa hii inatolewa, kulikuwa na Maaskofu 543, Mapadre 20,701; Watawa 33, 230 pamoja na Mashemasi wa kudumu 2,903.

Kuna waamini walei waliojiweka wakfu, ambao idadi yao imefikia 1,985 na Wamissionari walei ni 144, 910 na kuna Makatekista 483, 104. Waseminari walioko kwenye Seminari ndogo ni 2, 671 na Mafrateri ambao wanakaribia kupewa Daraja Takatifu la Upadre idadi yao ni 8, 956.

Kanisa Katoliki Brazil linawahudumia wanafunzi 1, 940, 299, wanaopata elimu kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu. Kuna vituo 3, 257 vinavyotoa elimu maalum. Kuna taasisi 5, 340 zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki au Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Brazil. Kuna jumla ya Hospitali 369, Kliniki 884 na vituo vya huduma kwa wakoma ni 22; kuna nyumba za wazee na wasiojiweza 718. Watoto yatima na walemavu wanahudumiwa kwenye vituo 1, 636. Mwishoni, Kanisa Katoliki nchini Brazil lina vituo 1, 711 kwa ajili ya kutoa ushauri nasaha kwa familia sanjari na kuenzi Injili ya Uhai.

Kwa ufupi, hii ndiyo sura ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Brazil, wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya kumpokea Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani inayofanyika huko mjini Rio de Janeiro.








All the contents on this site are copyrighted ©.