Hapa si suala la malumbano ya kisiasa na kidini, bali ni mambo yanayogusa utu na heshima
ya binadamu!
Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanakabiliwa na changamoto ya kusimama kidete
kulinda na kutetea Injili ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa
mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Maisha ni kati
ya tunu msingi ambazo watu wengi waliziheshimu na kuzithamini, lakini katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, uhai wa binadamu si mali kitu!
Lakini, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua na kuthamini utakatifu wa
maisha kwani unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, kuna uhusiano
wa pekee kwani mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, jambo linaloonesha uhusiano
wa pekee kati ya Mungu na binadamu. Kumbe, hili si suala la mapambano kati ya wanaharakati
na Kanisa au wanasiasa na Kanisa, bali ni mada inayogusa utu na heshima ya binadamu
kwani sera za utoaji mimba ni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na ni kinyume cha
haki msingi za binadamu. Uhai ni haki ya kila binadamu na kwamba, haki hii haiwezi
kutengeliwa na wanaharakati au wanasiasa.
Mama Kanisa anadhamana na wajibu
wa kusimama kidete kutetea Injili ya Uhai kwani ni sauti ya wanyonge na kwamba, kila
mtu anayo dhamana na wajibu wa: kuheshimu, kulinda, kupenda na kuhudumia Injili ya
Uhai; kwa kukataa katu katu kukumbatia Utamaduni wa kifo. Kuna maendeleo makubwa ya
sayansi na huduma ya dawa; mambo yanayopania kulinda na kuboresha afya ya binadamu,
lakini inasikitisha kuona kwamba, hata katika maendeleo haya Utamaduni wa kifo unaendelea
kushika kasi ya ajabu, kiasi kwamba, Uhai wa binadamu umekuwa ni kama kichokoo ambacho
watu wanaweza kukichezea kama wanavyopenda.
Hii ni sehemu ya tafakari ya kina
kutoka kwa Askofu mkuu Michael Neary katika Maadhimisho ya Siku ya Injili ya Uhai,
iliyofanyika hivi karibuni Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland. Ni wajibu na dhamana
ya Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni wa
Kifo, kwani huu ni wajibu msingi wa kimaadili kama ilivyo pia kwa dini kubwa duniani.
Injili ya Uhai inawagusa wote; mama na mtoto ambaye bado yuko tumboni mwake,
kwani tumbo la mama ni nyumba ya kwanza ya binadamu. Ni mahali ambapo mtoto anaanza
kuonja upendo na furaha kutoka kwa wazazi wake. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote
wenye mapenzi mema kutambua mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu hatari inayoweza
kuwepo kati ya maisha ya mama na mtoto! Lengo kuu daima liwe ni kwa ajili ya kuokoa
maisha ya binadamu na wala si kutaka kuyaangamiza kwa makusudi kutokana na ubinafsi.
Hakuna sheria ya utoaji mimba inayolenga kuokoa maisha ya binadamu!
Baraza
la Maaskofu Katoliki Ireland linabainisha kwamba, sheria ya utoaji mimba nchini humo
ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kimaadili. Kanisa bado linaendelea kushikamana
na kuwaonjesha huruma wale ambao wanasikitika mara baada ya kushiriki katika tendo
la utoaji mimba; linajitaidi kuwaelewa wale ambao wanakabiliwa na maamuzi machungu
kuhusu suala zima la utoaji mimba pamoja na kuwasaidia wale wote wanaoamua kuenzi
Injili ya Uhai.
Maaskofu Katoliki kutoka Ireland wanasema wanasukumwa na msimamo
wao wa kiimani kuthibitisha kwamba, kila haki msingi ya binadamu, ustawi na maendeleo
ya binadamu kwa siku za usoni inatokana na uelewa kwamba maisha ni kito cha thamani,
ni matakatifu na ni zawadi kutoka kwa Mungu; changamoto kwa kila mtu kukumbatia Injili
ya Uhai.