2013-07-18 10:00:54

Hongera Mzee Madiba!


Jumuiya ya Kimataifa imeadhimisha Siku ya Nelson Mandela Kimataifa kwa sala na shughuli mbali mbali kwa muda wa dakika 67, muda ambao Mzee Madiba aliutumia kwa ajili ya huduma kwa wananchi wa Afrika ya Kusini. Ni kielelezo makini cha kiongozi ambaye amejipambanua kwa kupinga ubaguzi wa rangi, nyanyaso na dhuluma, kiasi cha kusimama kidete kuanzisha mchakato wa upatanisho, haki na amani.

Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini anasema kwamba, hali ya Mzee Madiba bado si shwari sana. Amewashukuru wananchi wa Afrika ya Kusini na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake kwa kumsindikiza Mzee Madiba kwa sala, tangu alipolazwa Hospitalini hapo tarehe 8 Juni 2013.

Rais Barack Obama wa Marekani ni kati ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waliotuma salam na matashi mema kwa Mzee Madiba anapoadhimisha Miaka 95 tangu alipozaliwa. Anasema, anaikumbuka ziara yake aliyoifanya hivi karibuni Nchini Afrika ya Kusini na kwamba, aliguswa zaidi alipotembelea Kisiwa cha Robben, mahali ambako Mzee Nelson Mandela alifungwa kizuizini kwa miaka 27.







All the contents on this site are copyrighted ©.