Tarehe 18 Julai 2013 Mzee Madiba anatarajiwa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 95 tangu
alipozaliwa. Familia ya Mzee Nelson Mandela inasema kwamba, kwa vile Mzee Madiba hali
yake bado ni tete tangu alipolazwa Hospitalini takribani mwezi mmoja uliopita hawatakuwa
na maadhimisho ya kukata na shoka!
Siku ya Nelson Mandela itaadhimishwa nchini
Afrika ya Kusini na sehemu mbali mbali duniani ili kukumbuka mchango mkubwa uliotolewa
na Mzee Madiba katika mapambano dhidi ya sera za ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.
Umoja wa Mataifa, kunako mwaka 2009 ulitangaza kwamba, tarehe 18 Julai ya kila Mwaka
itakuwa ni Siku ya Mandela. Mwaka huu "Mandela Day" Inaadhimishwa wakati ambapo Mzee
Madiba anaendelea kupambana na mauti!
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana
Ban Ki-Moon anapenda kutoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuhakikisha kwamba, inafanya
kumbu kumbu kama njia ya kuendelea kumuenzi Mzee Madiba, kutokana na mchango wake,
uliopelekea maboresho makubwa si tu nchini Afrika ya Kusini, bali duniani kote!