2013-07-16 08:28:44

SECAM, hatuwezi kukaa kimya wakati wananchi wa Bara la Afrika wanaendelea kuteseka, kunyanyasika na kudhulumiwa!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, limehitimisha mkutano wake wa kumi na sita, uliofunguliwa hapo tarehe 9 hadi 14 Julai 2013 kwa kuwataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua zitakazosaidia maboresho ya maisha ya wananchi wa Bara la Afrika, badala ya mwelekeo wa sasa ambao umelifanya Bara la Afrika kuwa kama "kichwa cha mwenda wazimu" kila mtu akifika anataka kupora raslimali na utajiri wa Bara la Afrika kwa ajili ya mafao binafsi.

Mkutano mkuu wa SECAM umeongozwa na kauli mbiu "Kanisa kama Familia ya Mungu Barani Afrika katika huduma ya upatanisho, haki na amani". Mkutano umebainisha dira na mwelekeo wa utekelezaji wa Maazimio ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika pamoja na Waraka wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Dhamana ya Afrika.

Maaskofu wa SECAM wanawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema Barani Afrika, kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda na kutetea haki jamii, usawa, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Wajumbe wamezitaka Serikali Barani Afrika kusitisha vita inayoendelea kuleta maafa makubwa sanjari na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu. Wanasema, umefika wakati wa kuweka mikakati itakayosaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa upatanisho, haki na amani kwa ajili ya mafao ya wengi.

Katika mateso na mahangaiko ya watu wengi Barani Afrika, Maaskofu wa SECAM wanasema, kamwe hawataweza kukaa kimya, kwani vita na mahangaiko ya watu wengi wa Afrika inaonekana kusahaulika machoni pa Jumuiya ya Kimataifa. SECAM inawaomba viongozi wa kimataifa kuyavalia njuga matatizo ya Bara la Afrika ili kupata ufumbuzi wa kudumu.

Wajumbe wa SECAM wamesikitishwa na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kujitokeza huko: Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nchi zilizoko kwenye Pembe ya Afrika, Mali, Nigeria, Sudan ya Kusini, Madagascar, Rwanda, Uganda, Tunisia na Misri.









All the contents on this site are copyrighted ©.